Na mwandishi wetu
Uongozi wa Azam FC umesema sababu ya kucheza mechi ya kirafiki na Gor Mahia ya Kenya ni kukipa kikosi chao utayari wa kukabiliana na mechi za Ligi Kuu NBC zilizosalia kukamilisha ngwe ya kwanza.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa timu hiyo, Thabiti Zakaria, alisema wameichagua Gor Mahia kwa kuwa wanaamini ndiyo timu pekee itakayowapa mazoezi mazuri kuelekea mechi sita zilizobaki kumaliza mzunguko wa kwanza ligi kuu.
“Gor Mahia ndio mabingwa watetezi wa Kenya lakini pia wanafanya vizuri kwenye ligi yao ya FKF, siyo kwamba hapa nyumbani hakuna timu za kucheza nazo lakini nyingi zenye ubora ndio tunakutana nazo kwenye mechi za ligi ndio sababu tukaona twende Kenya,” alisema Zakaria.
Alisema mchezo huo utachezwa Nairobi, Novemba 19 na kikosi chao kitaondoka Dar es Salaam, Novemba 18, mwaka huu na timu itarudi nchini baada ya mechi hiyo ili wachezaji wapate muda wa kujiandaa na mchezo unaofuata dhidi ya Mtibwa Sugar.
Pia Zakaria alisema mechi hizo wanazozicheza watazitumia kama maandalizi ya kuikabili Simba mchezo ambao wanatarajia kucheza siku chache baada ya kumalizana na Mtibwa Sugar Novemba 24, mwaka huu.
Kwenye ligi Azam inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 19 sawa na Simba lakini iko juu kutokana na wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.
