Na mwandishi wetu
Makocha wa zamani wa soka nchini wamesema Yanga ilistahili kuibuka na ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Simba kutokana na ubora na uimara wa kikosi walichokuwa nacho msimu huu.
Akizungumza na GreenSports, Abdallah Kibadeni aliyewahi kuwa kocha na mchezaji wa zamani wa Simba alieleza kuwa Yanga walistahili ushindi huo kutokana na kuwa bora katika maeneo mengi ndani ya uwanja.
Kibadeni anayeshikilia rekodi ya kufunga mabao matatu katika mechi za watani wa jadi alisema eneo kubwa ambalo liliiletea tabu Simba ni safu ya kiungo ya Yanga ambayo ina wachezaji wenye ubunifu wa hali ya juu, kitu ambacho kocha wa Simba alishindwa kubaini hilo.
“Lazima tuseme ukweli Yanga walistahili ushindi tena wa idadi kubwa zaidi ya mabao kutokana na ubora wa kikosi walichokuwa nacho ukilinganisha na Simba ambao wanaonekana kukosa mbinu bora kutoka kwa benchi la ufundi,” alisema Kibadeni.
Maneno ya nguli huyo yameungwa mkono na aliyewahi kuwa mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Aden Rage ambaye amewataka Simba waache kutafuta mchawi badala yake watengeneze timu yenye uwezo wa kupambana na Yanga.
Rage alisema Yanga kwa sasa ina kikosi bora na ushindi wao haukuwa wa bahati na kilichoiponza Simba ni wachezaji wake wa safu ya ulinzi kufanya makosa mengi mbele ya washambuliaji wa Yanga wenye uwezo mkubwa wanapokuwa mbele ya lango la mpinzani.

“Tuwapongeze Yanga, walistahili ushindi, walicheza vizuri kuliko Simba na walizitumia vizuri nafasi walizotengeneza hasa kipindi cha pili kwa hiyo tuwapongeze na Simba tukajipange na kurekebisha makosa yetu,” alisema Rage ambaye pia aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa FAT sasa TFF.
Kocha na mchezaji wa zamani wa Yanga, Charles Mkwasa alisema kilichoiponza Simba kupoteza mchezo huo ni makosa mengi ambayo yalifanywa na safu yao ya ulinzi ambayo yalitoa nafasi kwa wachezaji wa Yanga kufunga mabao hayo.
Mkwasa amekiri Yanga ilistahili ushindi huo lakini hiyo imetokana na mbinu bora alizotumia kocha wao, Miguel Gamondi na ubora waliokuwa nao washambuliaji wa Yanga.
“Yanga walistahili kushinda kutokana na makosa mengi ambayo yalifanywa na wachezaji wa Simba, lakini inatokea sababu huo ni mchezo mkubwa wenye presha, pengine wachezaji wa Simba walikuwa na presha kubwa hatuwezi kujua lakini nimependa timu zote mbili zilionesha mchezo mzuri hata Simba pamoja na kwamba wamepoteza mchezo,” alisema Mkwasa.
