London, England
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta amesema bao pekee la ushindi la Newcastle dhidi ya timu yake lililofungwa na Anthony Gordon ni fedheha na aibu katika Ligi Kuu England (EPL).
Katika mechi hiyo iliyochezwa jana Jumamosi, Gordon alifunga bao hilo pekee katika dakika ya 64 na mwamuzi Stuart Attwell kulikubali baada ya kutumia VAR na hivyo kuifanya Arsenal ilale kwa bao 1-0.
VAR ilitumika kujiridhisha kwa matukio matatu kwanza ni kama mpira ulitoka nje ya uwanja, au Joelinton alicheza rafu kwa kumsukuma beki wa Arsenal, Gabriel na ama Gordon alikuwa eneo la kuotea.
Baada ya kutumia muda mrefu kufanya mapitio ya VAR, bao la Gordon lilikubaliwa na Newcastle kupata ushindi huku Arsenal ikipata pigo kwa kupoteza mara ya kwanza mechi ya EPL msimu huu.
“Ni jambo ambalo huwezi kuliamini kama tunalazimika kuzungumza kuhusu matokeo, tunalazimika kuzungumza kuhusu maajabu ya vipi hili linabaki kuwa goli, naona aibu,” alisema Arteta akiwa mwenye hasira mara baada ya mechi.
“Ni dhahiri kabisa bao hili kukubaliwa ni fedheha, sio goli kwa sababu nyingi tu, kwa goli kuruhusiwa kuna mambo ya kuangalia kabla ya hapo, kuna mambo yasiyoruhusiwa kwenye soka, iwe ni hapa, China, Japan au Ureno,” alisema Arteta.
Arteta alisema kwamba taratibu zilizopitiwa hadi kulikubali goli la Newcastle ni mfano mwingine wa ligi kuu kuharibiwa hadhi yake na tafsiri inayotokana na VAR.
“Kuna mengi ya kuangalia, ni vigumu mno kushindana katika mazingira kama haya, ni aibu, nimekuwa katika hii nchini kwa miaka zaidi ya 20 na ligi ya hapa haijakaribia japo kidogo katika kiwango cha ligi bora duniani,” alisema Arteta.
“Sijali nini watasema watu wa ligi kuu, wamechelewa mno, ni lazima nisimame hapa na kuelezea, tumepoteza pointi tatu, kuna mengi yenye utata, ni aibu,” alisema Arteta.
Kwa upande wake kocha wa Newcastle, Eddie Howe alisema kwamba lilikuwa goli zuri lakini alikiri kwamba taratibu nzima za kufikia uamuzi wa kulikubali goli zilikuwa na utata.
Matumizi ya VAR katika mechi za EPL yamekuwa yakishutumiwa mara kwa mara katika msimu huu kutokana na utata ambao umekuwa ukijitokeza.
