London, England
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta amekubali kubeba lawama baada ya timu yake kufungwa mabao 3-1 na West Ham na kutolewa katika michuano ya Carabao.
Katika mechi hiyo iliyochezwa jana Jumatano usiku, kocha huyo alifanya mabadiliko ya wachezaji sita katika kikosi chake cha kwanza akiwaweka benchi, Declan Rice, Bukayo Saka na nahodha Martin Odegaard.
“Nimekatishwa tamaa na ninahusika katika hili,” alisema Arteta akikubali kubeba lawama kwa kikosi alichokipanga ambacho hakikumpa matokeo mazuri.
“Tumetolewa katika mechi ya kikombe, nimekatishwa tamaa, tulitaka kucheza kwa namna tofauti lakini tulishindwa kufanya hivyo, wakati wote tunapopoteza mechi maumivu yako pale pale,” alisema Arteta.
“Tunalazimika kutumia maumivu haya na kufungwa huku kujiandaa kwa mechi yetu ya Jumamosi ya ligi kuu dhidi ya Newcastle,” alisema Arteta.
West Ham ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao la dakika ya 16 ambalo Ben White alijifunga wakati akiokoa mpira uliopigwa na Jarrod Bowen.
Arsenal hata hivyo iliamka baada ya kuingia kwa bao hilo na kufanikiwa kuutawala vyema mchezo lakini walishindwa kuipenya ngome ya West Ham na kujikuta wakiadhibiwa dakika ya 50 kwa bao la Mohammed Kudus.
Mambo yaliwaharibikia Arsenal kwa mara nyingine katika dakika ya 60 walipoachikwa bao la tatu lililofungwa na Bowen baada ya kushirikiana vizuri na White.
Bao pekee la kufutia machozi la Arsenal lilipatikana dakika ya 90 mfungaji akiwa ni Ødegaard ambaye Arteta alimuingiza na mastaa wengine wa kikosi cha kwanza lakini hawakuweza kuiepusha Arsenal na kipigo.
Kwa ushindi huo West Ham sasa imefuzu hatua ya robo fainali ya michuano hiyo ikijiandaa kuivaa Liverpool.
Nayo Man United ililala kwa mabao 3-0 mbele ya Newcastle huku kocha wa timu hiyo ambaye timu yake imekuwa na matokeo mabaya, Erik ten Hag akiahidi kuendelea kupambana licha ya mambo kwenda kombo.
Matokeo ya mechi za Carabao Jumatano hii…
West Ham 3-1 Arsenal
Bournemouth 1-2 Liverpool
Chelsea 2-0 Blackburn
Everton 3-0 Burnley
Ipswich 1-3 Fulham
Man Utd 0-3 Newcastle
kocha umetukeraaa sana ss mashabiki