Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliviera ‘Robertinho’ amesema atatumia siku chache zilizobaki kabla ya kuwakabili Yanga kuimarisha kikosi chake hasa safu ya ulinzi ambayo imekuwa na makosa ya kujirudia.
Alisema hayo akiwa kwenye maandalizi ya kuikabili Yanga Jumapili hii kwenye mchezo wa Ligi Kuu NBC utakaochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
“Malengo yetu ni kukusanya pointi tatu kwenye kila mchezo, hiyo ni mechi muhimu kwetu kushinda, tunaenda kucheza na timu bora, hivyo lazima tujiandae vizuri na kuhakikisha tunapunguza makosa.
“Safu ya ulinzi inafanya kazi nzuri lakini ina makosa ambayo yanajirudia, nitatumia wakati huu wa maandalizi kuendelea kuwaelekeza jinsi ya kufanya ili kuhakikisha wanapunguza makosa kwenye mchezo ujao “ alisema Robertinho.
Katika hatua nyingine Robertinho amesema kuwa anafurahishwa na maendeleo ya winga wa timu hiyo, Luis Miquissone na Moses Phiri jinsi wanavyoimarika na kumuongezea uchaguzi kwenye kikosi cha kwanza.
“Phiri ameendelea kuimarika na kufunga mabao muhimu pindi anapopata nafasi, hii ni ishara nzuri kwenye kikosi changu, nahitaji kuwa na wigo mpana wa kufanya uchaguzi wa kikosi,” alisema Robertinho.
“Miquissone tangu arejee Simba naye amekuwa na maendeleo mazuri tayari ametoa pasi mbili za mabao kwenye michezo muhimu na ndio maana nimekuwa nikimpa nafasi ili azidi kuwa bora,” alisema Robertinho.
