Liverpool, England
Klabu ya Liverpool imeeleza kufahamu matatizo yaliyoikumba familia ya mshambuliaji wake, Luis Diaz (pichani) ambaye baba na mama yake walitekwa nchini Colombia ingawa mama yake alipatikana baadaye.
Rais wa Colombia, Gustavo Petro alisema kupitia mitandao ya kijamii kwamba mama wa Luis alipatikana Barrancas lakini baba yake bado anaendelea kusakwa.
Kwa upande wa Liverpool, taarifa ya klabu hiyo mbali na kueleza kufahamu kilichomsibu mchezaji huyo, pia imesisitiza kuwa suala hilo litaendelea kuwa lao na wanalipa kipaumbele.
“Matarajio yetu makubwa ni kwamba jambo hilo litamalizika kwa amani na mapema kadri itakavyowezekana,” ilieleza taarifa ya Liverpool.
Shirikisho la Soka Colombia nalo limetoa taarifa yake likionesha mshikamano kwa mshambuliaji huyo na familia yake na kuzitaka mamlaka za usalama kuchukua hatua haraka iwezekanavyo.
“Tunapenda kuelezea mshikamano wetu kwake na familia yote na tunaziomba mamlaka husika kuchukua hatua haraka iwezekanavyo ili kumaliza utata uliojitokeza,” ilieleza taarifa ya shirikisho hilo.
Liverpool baadaye Jumapili hii jioni itacheza mechi ya Ligi Kuu England (EPL) dhidi ya Nottingham Forest, mechi ambayo uwezekano wa Diaz kucheza ni mdogo mno.
