Na mwandishi wetu
Wachezaji nyota wa Yanga wamempongeza kiungo wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’ kwa kiwango kikubwa alichokionesha timu hizo zilipokutana jana Jumatatu kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam na Azam kufungwa mabao 3-2.
Wachezaji hao walioongozwa na kiungo wa Uganda, Khalid Aucho walitoa pongezi zao hizo kwenye chapisho la Fei aliloliweka jana kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram kwa kuweka picha ya mechi hiyo ya juzi.
Kwa upande wake Aucho aliandika kwenye maoni ya chapisho hilo: “Mchezo mzuri jana kaka endelea kupambana.”
Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Stephane Aziz Ki alimsifia Fei kwa kumwita mchezaji mkubwa, ambapo Fei aliujibu ujumbe huo kwa kushukuru na yeye kumpongeza Ki kwa uwezo wake akimwita “Master Ki”.
Wengine waliompongeza Fei ambaye msimu uliopita alikuwa akikipiga Yanga ni beki Ibrahim Bacca na mshambuliaji wa Pyramids ya Misri ambaye aliandika: “Zanzibar Finest ni mmoja tu.”
Mechi hiyo ya juzi ni mechi ya pili, Fei anakutana na waajiri wake hao wa zamani ambapo mechi ya kwanza ilikuwa ya Ngao ya Jamii mwanzoni mwa msimu huu na Azam ikafungwa mabao 2-0, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Hata hivyo, katika mechi hiyo ya juzi, Fei alionesha kiwango kikubwa na alionekana kuisumbua mno safu ya kiungo ya Yanga kiasi cha Aucho na Mudathir kuadhibiwa kwa kadi ya njano kutokana na kumchezea madhambi kiungo huyo.
Soka Wachezaji Yanga wampongeza Fei Toto
Wachezaji Yanga wampongeza Fei Toto
Read also
