Rio de Janeiro, Brazil
Rais wa Shirikisho la Soka Brazil (CBF), Ednaldo Rodrigues ameeleza kusikitishwa na muendelezo wa vitendo vya ubaguzi wa rangi dhidi ya mshambuliaji wa Real Madrid na timu ya taifa ya Brazil, Vinicius Junior.
Vinícius Jr (pichani juu) alikumbana na kadhia hiyo Jumamosi iliyopita katika mechi ya La Liga ambayo Real Madrid ilitoka sare ya bao 1-1 na Sevilla lakini baadaye picha za video zilimuonesha shabiki mmoja akitoa ishara za kibaguzi kwa mchezaji huyo katika dakika ya 86.
“Inasikitisha kuona matukio ya ubaguzi wa rangi yanafanyika kwa mara nyingine dhidi ya Vinícius Júnior,” alisema Rodrigues katika taarifa ya CBF.
“Ubaguzi wa rangi ni jinai na ni lazima upigwe vita kwa wakati wote, inasikitisha bado tunaona matukio ya aina hii, mimi ni mtu mweusi na najua maumivu anayoyapata Vinicius kwa kila matukio ya kibaguzi anayofanyiwa na mashabiki,” alisema Rodrigues.
“Kwa wakati wote nitaonesha mshikamano na wanaokumbana na kadhia ya ubaguzi wa rangi, hatuwezi kulirahisisha jambo hili, sauti yangu itasikika kwa wakati wote katika kukabiliana na vitendo hivi vya kikatili,” alisema Rodrigues.
Vinicius Jr, 23 amekuwa mlengwa wa kadhia za ubaguzi wa rangi kutoka kwa mashabiki wa timu pinzani, mapema mwezi huu alitoa ushahidi kwenye vyombo vya sheria dhidi ya mashabiki watatu wa klabu ya Valencia waliodaiwa kumtolea kauli za kibaguzi katika tukio la mwezi Mei.
Hivi karibuni Vinicius Jr alinukuliwa akisema kwamba vitendo vya ubaguzi wa rangi ni jambo la kawaida katika La Liga na timu pinzani zinashawishi vitendo hivyo.
Viongozi wa La Liga wameanzisha mfumo maalum ambao unayanasa matukio yote ya kibaguzi na wahusika kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
