Na mwandishi wetu
Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Gianni Infantino ameeleza furaha yake na kulipongeza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Tanzania kwa ujumla kwa busara inayotumika katika kukuza maendeleo ya soka nchini.
Infantino ameeleza hayo kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Instagram huku pia akimpongeza Rais wa Shirikisho Soka Afrika (Caf), Patrice Motsepe kwa kazi nzuri anayoendelea kuifanya.
“Ilikuwa furaha kuwa Tanzania na kuzindua miradi ya ya maendeleo ya Fifa Kigamboni na Tanga. Pongezi nyingi kwa Wallace Karia, Rais wa TFF na Patrice Motsepe, Rais wa Cad pamoja na jamii nzima ya mpira wa miguu katika nchi hii nzuri.
“Kila nchi duniani ambayo ni sehemu ya Fifa inapata fedha za kuwekeza kwenye maendeleo ya soka, lakini kuna baadhi ya nchi ambazo ni maalum sana, na zinawekeza fedha wanazozipata kwa busara na mtazamo wa mbele na hakika Tanzania ni mojawapo,” alisisitiza Infantino katika chapisho lake hilo.
Infantino ambaye alikuwa nchini kwa ajili ya uzinduzi wa michuano mipya ya African Football League (AFL) uliofanyika Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam Ijumaa iliyopita, alizipongeza timu za Simba na Al Ahly ya Misri kwa mchezo mzuri siku hiyo.
Kiongozi huyo wa Fifa pia aliwapongeza mashabiki walioonesha hisia na morali kubwa katika mechi hiyo iliyoisha kwa sare ya mabao 2-2.
“Kuzinduliwa kwa ligi mpya ya soka ya Afrika (AFL) ilikuwa tukio la kipekee kweli kweli! Hongera Simba SC na Al Ahly kwa mchezo mzuri pamoja na waamuzi kwa ubora wa kuchezesha. Shukrani nyingi kwa mashabiki kwa kuonyesha shauku, hisia na upendo kama huu,” alisema Infantino.
“Hili lilikuwa onyesho kamili la kandanda ya Afrika na jinsi AFL itakavyobadilisha mandhari hapa, kuweka kiwango cha maendeleo endelevu, ufikiaji na ushirikishwaji,” alifafanua Infantino.
