Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu Azam FC, Youssouph Dabo amewaeleza wachezaji wake kuonesha thamani yao ya juu katika kila mchezo ukiwemo dhidi ya Yanga utakaopigwa Jumatatu hii kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Dabo (pichani) ameeleza kuwa anawafahamu Yanga kwa kuwa alikutana nao kwenye mechi ya Ngao ya Jamii na kufungwa mabao 2-0 lakini anaamini hii ni mechi nyingine na amewaandaa wachezaji wake kiutofauti pia.
“Nimewaeleza wachezaji wangu tangu tumeanza msimu kwamba hatuchezi na mpinzani mmoja au wawili, tunapaswa kucheza vizuri kila wakati, kupambana na kuonesha thamani yetu kwa kushikamana na utayari kila mchezo, hilo ndio la muhimu.
“Na sasa tunakutana na Yanga, timu ambayo tulikutana nayo Tanga (Uwanja wa Mkwakwani) katika Ngao ya Jamii, ulikuwa wakati mzuri kuwafahamu lakini huu ni mchezo mwingine na kuna utofauti tangu wakati ule na sasa hivyo tunaendelea kujiandaa tukitazamia kukua zaidi kila wakati,” alisema Dabo raia wa Senegal.
Timu hizo zinakutana Azam ikiwa juu katika nafasi ya pili kwa pointi 13 baada ya ushindi wa mechi nne na sare moja wakati Yanga ipo nafasi ya tatu kwa pointi 12 ilizovuna baada ya ushindi wa mechi nne na kufungwa mchezo mmoja.
Licha ya upinzani uliopo baina ya timu hizo lakini mchezo huo unatarajia kuwa mkali kutokana na Azam kutaka kulipa kisasi huku Yanga ikihitaji ushindi ili ikae juu iendelee kupigania kutetea ubingwa wake iliotwaa mara mbili mfululizo.