Na mwandishi wetu
Kocha mpya wa Ihefu, Moses Basena amesema anahitaji wiki mbili kuisuka upya timu hiyo ili kuwa na mwenendo mzuri kwenye Ligi Kuu NBC.
Akizungumza na GreenSports, kocha huyo raia wa Uganda alisema hiyo ni kutokana na mapungufu aliyoyakuta kwa wachezaji na ushindani uliopo kwenye ligi ya msimu huu.
“Tuna wachezaji wazuri lakini kwa siku chache nilizokuwa hapa nimebaini ambacho ndio nakifanyia kazi kwenye mazoezi yetu, naamini baada ya muda mfupi tutakuwa tayari kuwapa furaha mashabiki zetu kila tutakapocheza,” alisema Basena.
Kocha huyo ambaye amechukua nafasi ya Zuberi Katwila, alisema malengo yake ni kuifanya Ihefu kuwa timu inayopigania ubingwa na siyo kusindikiza timu nyingine.
Alisema uongozi wa timu hiyo umemuahidi kumpa kila atakachohitaji ili kutimiza lengo hilo na yeye atahakikisha anafanikisha hayo kwa kujenga kikosi imara kitakachopigania ubingwa wa ligi kuanzia msimu huu.
Alisema hilo linawezekana sababu ligi ndio imeanza hivyo ana muda wa kutosha kurekebisha mapungufu yaliyopo na kujenga kikosi cha ushindani.
Basena aliyewahi kukinoa kikosi cha Simba mwaka 2011 kabla ya kutua Ihefu alikuwa kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Uganda maarufu kwa jina la The Cranes.
