Na mwandishi wetu
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo Tanzania, Ally Mayay (pichani) amewataka viongozi TFF kurejesha utaratibu wa kuujulisha umma na mashabiki wa soka Tanzania juu ya kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars kila kinapoitwa kambini.
Mayay ameeleza hayo alipokuwa akihojiwa na kituo kimoja cha televisheni nchini ikiwa ni takriban mara ya pili mfululizo kikosi hicho kinaitwa kimyakimya bila ya uwepo wa taarifa rasmi.
Hivi karibuni kikosi cha Stars kilichokuwa kikijiandaa kwa mechi ya kirafiki dhidi ya Sudan kiliitwa kimya kimya.
“Ni kweli kila kocha anakuwa na mipango yake lakini ifahamike hii ni timu ya taifa kama inavyoelezwa ni ya Watanzania na wanahabari wanahitaji pia kufahamu kikosi kwa ajili ya kutoa sapoti. Na inatoa urahisi kwa wapenzi na mashabiki maana wanapenda kujua wachezaji walioitwa iwe rahisi kwao kufahamu taarifa zao na kufuatilia wachezaji wao.
“Na mashabiki wengi wa Tanzania wanasapoti timu zao kama vile Simba, Yanga, sasa linapokuja suala la taifa mashabiki wana haki hiyo ya kupata taarifa za timu ya taifa kwa ajili ya kwenda kuisapoti, kama hivyo tunajiandaa kwa Afcon (Michuano ya Mataifa Afrika) mwakani, hivyo inapaswa tupeane taarifa ili kuwa pamoja katika mipango kama hii ya kuelekea Afcon,” alisema Mayay mchezaji wa zamani wa Stars.
Mayay alisema inapaswa mashabiki kupewa wanachostahili kwani hata serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imekuwa mstari wa mbele kutoa sapoti ya fedha kwa timu za taifa hivyo mashabiki wake ambao ni Watanzania wana uhalali wa taarifa za timu hiyo.
“Naamini Shirikisho la Soka (TFF) litafanyia kazi suala hilo ili kurejesha utaratibu ule ule wa kutoa taarifa mapema ili watu pia wafanye uchambuzi sababu hata uchambuzi unaofanywa na media huwa na manufaa makubwa kwa kocha,” alisema Mayay.
