Na mwandishi wetu
Kiungo wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Baraka Majogoro amesema anashukuru Mungu kutimia kwa ndoto yake ya kucheza nje ya nchi huku akiamini sasa ni njia sahihi ya kutimiza malengo yake katika soka.
Mchezaji huyo anayekipiga Chippa United ya Ligi Kuu Afrika Kusini aliyojiunga nayo msimu huu akitokea KMC, amekuwa mchezaji tegemeo katika kikosi cha Chippa inayoshika nafasi ya saba ikiwa na pointi 13 katika mechi tisa.
“Ilikuwa ndoto na malengo yangu kwamba siku moja nicheze nje ya Tanzania, nashukuru Mungu amenijaalia ndoto imetimia na zaidi naomba anijaalie nitimize malengo yangu zaidi ya hapo,” alisema Majogoro aliyewahi kukipiga Mtibwa Sugar.
Awali, Majogoro alipojiunga na Chippa hakucheza katika mechi nne za awali za ligi ambazo walifungwa mbili na sare mbili lakini alipopangwa kwenye mechi iliyofuata timu hiyo ilipata ushindi wa kwanza wa bao 1-0 dhidi ya Cape Town Spurs na tangu hapo amekuwa na namba ya kudumu katika kikosi hicho.
Kiungo huyo pia ameeleza kuhusu michuano ya Afcon ambapo Tanzania imepangwa Kundi F dhidi ya Morocco, DR Congo na Zambia akifafanua kufahamu ubora na ubabe wa timu hizo lakini kama wakijiandaa vya kutosha kwa uzito wa michuano hiyo, anaamini wapinzani hao hawawezi kuwazuia kutimiza ndoto zao.
