London, England
Kocha wa timu ya taifa ya England, Gareth Southgate amesema hatojali tukio la kiungo wake Jordan Henderson kuzomewa na mashabiki katika uteuzi wa timu yake itakayocheza na Italia, leo Jumanne.
Ijumaa iliyopita, Henderson aliyekuwa nahodha katika mechi ya kirafiki dhidi ya Australia, alijikuta akizomewa na mashabiki wa England licha ya timu yake kutoka na ushindi wa bao 1-0.
Alipoulizwa kwenye mkutano na waandishi wa habari kama atampanga mchezaji huyo katika mechi hiyo ya kufuzu Kombe la Ulaya 2024 au Euro 2024 kama zomea zomea hiyo itaendelea, Southgate alijibu ndio atampanga.
“Ndio kwa asilimia 100, wakati wote huwa nachagua wachezaji ambao nafikiri ni wazuri kuiwakilisha timu, wachezaji ambao wanatupa nafasi nzuri ya kupata ushindi labda litokee jambo ambalo naona si sahihi,” alisema Southgate.
“Katika hili watu wanaweza wasikubaliane na msimamo wa Jordan au uamuzi wake kutokana na msimamo wa siku za nyuma wa kuunga mkono mapenzi ya jinsia moja, lakini sidhani kama hiyo inaweza kuwa sababu ya kutompanga kwenye timu au sababu ya kumzomea,” alisema Southgate.
Julai mwaka huu, Henderson alihamia Saudi Arabia katika klabu ya Al-Ettifaq inayoshiriki Ligi Kuu ya Saudi Arabia au Saudi Pro Ligi kwa mkataba wa miaka mitatu akitokea Liverpool ya England.

Uamuzi wa kuhamia Saudi Arabia umepewa tafsiri tofauti kwa kuwa mchezaji huyo amekuwa akiunga mkono mapenzi ya jinsia moja jambo ambalo ni haramu Saudi Arabia lakini pia baadhi ya mashabiki hawakubaliani na msimamo wake wa kuunga mkono mapenzi ya jinsia moja.
Henderson mwenyewe ameamua kuwapuuza mashabiki wanaomzomea wakati Southgate amesema kwamba hajaiona mantiki ya zomea zomea kwa mchezaji huyo.
