Doha, Qatar
Bilionea wa Qatar, Sheikh Jassim bin Hamad Al Thani (pichani) aliyekuwa akipewa nafasi kubwa ya kuinunua klabu ya Manchester United, amejitoa katika mpango huo.
Sheikh Jassim ambaye amewekeza katika mabenki, alitangaza dau la Pauni 5 bilioni lakini mazungumzo ya mpango huo yaliyofanyika mapema wiki hii yameshindwa kufikia muafaka katika suala hilo.
Hatua ya Sheikh Jassim kuonesha nia ya kutaka kuinunua klabu hiyo ilikuja baada ya Familia ya Glazer ambayo mwaka 2005 iliinunua klabu hiyo kwa Pauni 790 milioni, kutangaza mwaka jana mwishoni kwamba wanafikiria kuiuza.
Mtu pekee ambaye alionesha upinzani wa uhakika kwa Sheikh Jassim ni mfanyabiashara maarufu wa Uingereza, Sir Jim Ratcliffe kupitia kampuni yake ya Ineos na ambaye hapana shaka sasa atakuwa na nafasi zaidi ya kununua hisa nyingi.
Awali ilielezwa kuwa Ratcliffe alikuwa amepania kununua sehemu ya hisa katika klabu hiyo kwa lengo la kuondoa utaratibu wa mtu mmoja kuwa na hisa nyingi na hivyo kuwa na sauti kubwa katika mwenendo wa klabu.
Mara baada ya Familia ya Glazer kutangaza nia ya kuiuza klabu hiyo habari za ushawishi zimekuwa nyingi zikihusisha matajiri mbalimbali lakini waliojitokeza na kuonesha dhamira ya wazi ni Sheikh Jassim na Ratcliffe na kwa uamuzi wa Sheikh, Ratcliffe atakuwa na nafasi kubwa ya kununua hisa hizo.
Katika mipango ya Sheikh Jassim kuinunua klabu hiyo ilidaiwa kwamba pesa zake zingefuta madeni ya zamani, kungekuwa na pesa za ujenzi wa uwanja mpya, kununua wachezaji wa bei mbaya na miradi mingineyo ya maendeleo ya klabu.
Mashabiki wa Man United mara kadhaa wamekuwa wakiipinga Familia ya Glazer kwa maandamano ambayo yamekuwa yakifanyika nje ya Uwanja wa Old Trafford unaomilikiwa na klabu hiyo.
Man United kwa sasa inashika nafasi ya 10 kwenye Ligi Kuu England, tayari imepoteza mechi nne kati ya nane za mwanzo za ligi hiyo na imepokea kichapo katika mechi mbili za kwanza za Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kimataifa Sheikh afuta mpango kuinunua Man United
Sheikh afuta mpango kuinunua Man United
Read also
