Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amewatoa hofu mashabiki wa timu hiyo akisema kuwa kikosi chao kipo tayari kucheza na Al Ahly na kupata ushindi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Miamba hiyo ya soka tayari imeingia kambini kujiandaa na mchezo huo wa ufunguzi dhidi ya Al Ahly ya Misri ikiwa ni ufunguzi wa michuano mipya ya African Footbal League (AFL) inayoshirikisha timu nane pekee.
Robertinho alisema usajili walioufanya msimu huu pamoja na kushinda mechi tano mfululizo za Ligi Kuu NBC unaonesha namna gani walivyokuwa tayari kwa mchezo huo wa ufunguzi ambao utachezwa Oktoba 20, mwaka huu.
“Ni kweli ni mechi ngumu sababu tunacheza na bingwa wa Afrika, lakini ugumu huo hautokuwa kwetu, bali kwa timu zote mbili na Al Ahly wanalijua hilo, Simba hatujapoteza mechi nne za Afrika zilizopita, mashabiki wanapaswa kulijua hilo na wasimame mstari wa mbele kujivunia timu yao,” alisema Robertinho.
Kocha huyo alisema wana mbinu mbadala za kuwapa matokeo mazuri hasa wanapocheza na timu kubwa kama hiyo, hivyo haoni sababu ya mashabiki wao kuwa na hofu kwani uhakika wa ushindi kwenye uwanja wa nyumbani ni mkubwa tofauti na wanavyofikiria.
Alisema Simba ni timu kubwa na inaogopewa Afrika na wamedhamiria kuthibitisha hilo kwa kuifunga Al Ahly ili kujitengenezea mazingira mazuri ya kusonga mbele hatua zinazofuata kwenye mashindano hayo ya AFL.
Simba ambao kwa sasa wanashika usukani katika ligi kuu, wanashiriki michuano ya AFL, kutokana na ubora waliouonesha kwenye mashindano ya Caf katika kipindi cha miaka minne iliyopita.
