Abidjan, Ivory Coast
Tanzania imepangwa Kundi F katika fainali za Afcon 2023 ambalo pia lina timu ya Morocco na wakati mashabiki wakijiuliza kama timu hiyo itafuzu hatua ya mtoano, beki wa Morocco, Achraf Hakimi amesema timu yao inachotaka ni kubeba taji hilo.
Kwa mujibu wa droo iliyotangazwa Alhamisi hii usiku, wapinzani wengine wa Tanzania au Taifa Stars katika kundi hilo ni DR Congo na Zambia, timu ambazo ambazo zinatajwa kuwa ni nyepesi kwa Morocco.
Morocco ambayo mwaka jana iliweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza barani Afrika kufikia hatua ya nusu fainali ya Kombe la Dunia itakuwa pia ikiwania taji hilo kwa mara ya pili katika fainali zitakazopigwa mwakani nchini Ivory Coast.
“Tuna timu nzuri, kundi zuri na tutafanya kila tuwezalo kubeba taji, tutafanya kila kitu katika fainali hizi za Afcon, kama ambavyo tulifanya wakati wa fainali za Kombe la Dunia,” alisema Hakimi ambaye pia ni beki wa timu ya PSG ya Ufaransa.
Na ingawa Hakimi anaamini kuwa timu yao haitopata tabu kwenye Kundi F lakini anatambua uwapo wa vigogo katika bara la Afrika timu kama za Senegal na Misri ambazo zinaweza kuiweka katika wakati mgumu nchi hiyo kubeba taji hilo.

Fainali za Afcon zitaanza kutimua vumbi Januari 13 hadi Februari 17 mwakani ambapo viwanja sita vitatumika vikiwamo vitatu vipya vilivyojengwa katika miji ya Abidjan, Korhogo na San Pedro.
