London, England
Kocha mpya wa timu ya Birmingham, Wayne Rooney amesema kwamba anaamini timu hiyo inatakiwa kuwa kwenye Ligi Kuu England (EPL) na lengo lake ni kufanikisha jambo hilo.
Rooney, 37, aliyekuwa kocha wa timu ya D.C United ya Marekani, ametangazwa rasmi juzi Jumatano kuinoa timu hiyo inayoshiriki ligi ya Championship kwa mkataba wa miaka mitatu na nusu.
“Nataka kuijenga Birmingham, haipo mahali ambapo ilikuwa kwa miaka 10 iliyopita na sasa hii ni changamoto na fursa ya kuirudisha huko,” alisema Rooney nahodha na mshambuliaji wa zamani wa timu ya taifa England.
Uamuzi wa kumpa Rooney majukumu ya kuinoa Birmingham umechukuliwa na wamiliki wapya wa klabu hiyo, Shelby Companies Limited (SCL) wa nchini Marekani ambao waliamua kuachana na kocha John Eustace aliyeinoa timu hiyo kwa takriban miezi 15.
Birmingham kwa sasa inashika nafasi ya sita kwenye ligi ya Championship ambapo mtihani wa kwanza wa Rooney na timu hiyo utakuwa Oktoba 21 katika mechi dhidi ya Middlesbrough, timu inayonolewa na mchezaji mwenzake wa zamani wa Man United, Michael Carrick.
Rooney ambaye pia amewahi kuichezea Everton, tayari amefanya kikao na wachezaji wa timu hiyo na kuelezea ubora wa wachezaji vijana waliopo, wachezaji ambao amesema anaweza kuwaendeleza kwani hilo jambo ambalo amekuwa akijaribu kulifanya wakati wote tangu awe kocha.
