Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amesema hataki kuongea lolote kuhusu mechi za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, sababu akili yake ipo kwenye mchezo unaofuata wa Ligi Kuu NBC dhidi ya Azam FC.
Oktoba 25, mwaka huu Yanga itakuwa mwenyeji wa Azam FC mchezo unaotarajiwa kuwa na upinzani mkali kutokana na ushindani na uimara wa vikosi vya timu zote mbili.
Gamondi raia wa Argentina alisema lengo lake kubwa ni kuhakikisha Yanga inarudi kileleni mwa msimamo wa ligi baada ya kuondolewa kwenye nafasi hiyo kufuatia kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Ihefu FC.
“Bado kuna kilometa nyingi kufikia mechi za makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kwa sasa akili yangu inaupigia hesabu mchezo uliopo mbele yetu dhidi ya Azam sababu ndio utatupa picha ya kusudio letu la kurudi kwenye uongozi wa ligi,” alisema Gamondi.
Kocha huyo raia wa Argentina alisema anaufikiria mchezo huo kwa kuwa Azam ni moja ya timu bora kwenye ligi ya Tanzania na imekuwa na matokeo mazuri tangu kuanza kwa msimu ndio maana wapo juu yao kwa tofauti ya pointi moja.
Yanga ambao ndio mabingwa watetezi wa taji hilo la Ligi Kuu NBC wapo nafasi ya tatu wakiwa na pointi 12, Azam ipo nafasi ya pili na pointi zao 13 na Simba ndio vinara kwenye msimamo wa ligi wakikusanya pointi 15 baada ya kushinda mechi zote tano walizocheza.
