Na mwandishi wetu
Bondia wa ngumi za kulipwa, Hassan Mwakinyo ‘Champez’ ameeleza kutokukubaliana na adhabu ya kufungiwa kukaa nje ya mchezo huo kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Mwakinyo ameeleza hayo leo Jumatano akiiambia GreenSports kuwa kwa sasa angependa kuwatoa hofu mashabiki wake kwamba wasishtushwe na walichokisikia, kwani ndani ya siku saba alizopewa za kukata rufaa juu ya hilo, atatoa tamko lake rasmi.
“Binafsi nisingependa kuongelea hilo kwa sasa lakini niwatoe hofu mashabiki wangu kwamba kufungiwa haiwezekani. Mashabiki wasubiri kuona kwamba kwanini nimesema haiwezekani, sio kitu naweza kuzungumza sasa hivi hapa lakini watapata majibu kabla ya siku saba nilizopewa kuisha.
“Kama haki itafanya kazi maana yake si ushindi sababu sina makosa katika hilo na kama nitaamua kukata rufaa na kubainika nina makosa kweli, basi nifungiwe maisha na sio mwaka na kama itabainika sina makosa, waliotengeneza makosa nao pia wafungiwe vilevile,” alisema Mwakinyo.
Jana Jumanne, Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC) ilitangaza kumfungia kwa mwaka mmoja bondia huyo kwa kosa la kutopanda ulingoni Septemba 29, mwaka huu.
Pambano hilo lililopangwa kupigwa kwenye Ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam kuwania mkanda wa IBA dhidi ya Mnamibia, Julius Indongo, Mwakinyo alikataa kupigana kwa alichoeleza kuwa ni udanganyifu na kukiukwa kwa makubaliano ya msingi na promota wake wa pambano hilo.
TPBRC ilieleza adhabu hiyo pamoja na faini ya Sh milioni moja imetokana na Mwakinyo kuchukua uamuzi pasi na kuheshimu mkataba, kitendo ambacho hakina afya kwa ndondi nchini na kwa ukubwa alionao alipaswa kuonesha mfano kwa mabondia chipukizi huku akipewa nafasi ya kukata rufaa ya adhabu hiyo ndani ya siku saba.
