Na mwandishi wetu
Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC) imetangaza kumfungia bondia Hassan Mwakinyo kwa mwaka mmoja kwa kosa la kutopanda ulingoni Septemba 29, mwaka huu kupambana na Julius Indongo.
TPBRC kupitia kamati yake ya nidhamu imetangaza hayo leo Jumanne, kwamba imefikia uamuzi huo baada ya kumsikiliza Mwakinyo na Kampuni ya PAF ambayo ni promota wa pambano hilo lililotarajiwa kupigwa Ubungo Plaza, Dar es Salaam kuwania mkanda wa IBA.
Katibu Mkuu wa TPBRC, George Lukindo alisema kufungiwa huko kunakwenda sambamba na adhabu ya Sh milioni moja huku Mwakinyo akiwa na nafasi ya kukata rufaa juu ya maamuzi hayo ndani ya siku saba.
“Chini ya kamati ya nidhamu tulipata maelezo ya pande zote mbili kutoka Kampuni ya PAF na Mwakinyo, watueleze kwa nini Mwakinyo hakupanda ulingoni. Kamati iliona sababu za Mwakinyo hazina mashiko na amekiuka mkataba wake na Kampuni ya PAF.
“Msingi mkuu wa kutoa adhabu hiyo ni sababu Mwakinyo ni bondia mkubwa Tanzania, angepaswa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha anakuwa mfano bora kwa mabondia chipukizi na kitendo chake cha kuchukua uamuzi pasi na kuheshimu mkataba hakina afya kwa maslahi ya maendeleo ya ngumi za kulipwa nchini,” alisema Lukindo.
Mwakinyo hakupanda jukwaani kwa alichoeleza ni udanganyifu na kukiukwa kwa makubaliano ya msingi na promota wake juu ya ushirikiano wao na kampuni nyingine zilizokuwa tayari kusimamia pambano hilo.
