Na mwandishi wetu
Simba SC imeeleza kuwa hadi sasa haijatoa tuzo ya mchezaji bora wa mwezi msimu huu kutokana na kukosekana kwa mdhamini wa tuzo hizo.
Kwa miaka miwili iliyopita, Simba kila mwezi katika miezi inayochezwa ligi imekuwa ikitoa tuzo ya mchezaji bora wa mashabiki wa timu hiyo iliyokuwa ikidhaminiwa na Kampuni ya Emirate Aluminium ACP.
Meneja Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally ameiambia GreenSports leo Ijumaa kuwa kampuni hiyo imemaliza mkataba wake msimu uliopita ndio maana kwa sasa hazisikiki tena tuzo hizo zilizokuwa zikipigiwa kura na mashabiki wa Wekundu hao.
“Mkataba wetu na kampuni iliyokuwa ikidhamini tuzo hizo umemalizika tangu mwishoni mwa msimu uliopita ndio maana hazionekani kwa sasa, maana ile tuzo huwa ni zawadi ya mdhamini kwa mchezaji aliyefanya vizuri ndani ya mwezi,” alisema Ally.
Ally pia alibainisha kuwa milango ipo wazi kwa kampuni inayotaka kufanya hivyo kama ilivyofanya Emirate Aluminium Septemba 21, mwaka juzi kwa kusaini mkataba wa Sh milioni 300 kwa ajili ya dili hilo.
