Na mwandishi wetu
Simba imeishusha Yanga kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu NBC huku ikiendeleza rekodi ya ushindi katika ligi hiyo kwa kuichapa Prisons mabao 3-1 katika mechi iliyopigwa Ahamisi hii kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Ushindi huo sasa umeifanya Simba kufikisha pointi 12 ikiwa imeendelea kupata ushindi katika mechi yake ya nne mfululizo bila kupoteza hata mechi moja tangu kuanza kwa ligi hiyo.
Yanga iliyokuwa ikiongoza ligi hiyo ilikwama jioni ya Jumatano baada ya kulala kwa mabao 2-1 mbele ya Ihefu na hivyo kubaki na pointi zake tisa.
Prisons waliouanza mchezo huo kwa kasi huku wakishangiliwa na mashabiki, walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 12 lililofungwa na Edwin Balua kwa mpira wa adhabu baada ya Balua kuchezewa rafu na beki wa Simba, Che Malone.
Shangilia ya mashabiki ilizidi kushika kasi pengine kutokana na imani kwamba kilichoikuta Yanga dhidi ya Ihefu kingeikuta Simba katika lakini timu hiyo ilitulia na kuanza kusaka bao la kusawazisha juhudi zilizozaa matunda dakika ya 34 kwa bao lililofungwa na Clatous Chama akiitumia vizuri pasi ya Shomary Kapombe.
Dakika chache kabla ya mapumziko, nahodha John Bocco alishindwa kuitumia nafasi nzuri kuipatia Simba bao baada ya kupiga shuti ‘lisilo na macho’ lakini mshambuliaji huyo alirekebisha kosa hilo dakika ya 45 kwa kuujaza mpira wavuni akiitumia pasi ya Muzamir Yassin.
Simba iliandika bao la tatu katika dakika ya 54 mfungaji akiwa ni Saido Ntibanzokiza aliyeujaza mpira wavuni kwa mkwaju wa penalti ambayo ilitolewa baada ya Mosses Phiri kufanyiwa madhambi na kipa wa Prisons, Yona Amos.
Katika mechi hiyo timu zote zilifanya mabadiliko, Prisons iliwatoa, Lambert Sibiyanka, Meshack Seleman na Mambote Batshi na nafasi zao kuingia Messi Roland, Zabona Khamis na Samson Mbangula.
Kwa upande wa Simba nayo iliwatoa Dennis Kibu, Ntibazonkiza, Bocco na Chama na nafasi zao kuchukuliwa na Onana, Kanoute, Phiri na Chilunda.
Soka Simba yaishusha Yanga kileleni
Simba yaishusha Yanga kileleni
Read also
