Manchester, England
Winga wa Man United, Antony anayetuhumiwa kwa kosa la kumdhalilisha mpenzi wake, huenda leo akaichezea timu yake katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Galatasaray ya Uturuki.
Antony alionekana kwa mara ya mwisho akiiwakilisha Man United, Septemba 3 katika mechi dhidi ya Arsenal na baada ya hapo alilazimika kujiweka kando baada ya aliyekuwa rafiki yake wa kike Gabriela Cavallin kuibuka na tuhuma hizo.
Katika kipindi hicho hicho, Antony pia aliachwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Brazil kilichokuwa kikijiandaa kwa mechi za kufuzu Kombe la Dunia 2026.
Antony hata hivyo alirejea mazoezini kwenye kikosi cha Man United kwa mara ya kwanza Jumapili, hiyo ni baada ya kuripoti polisi na kuhojiwa kabla ya kuachiwa bila kufunguliwa kesi katika tuhuma zinazomkabili.
Kocha wa Man United, Erik ten Hag alisema kwamba mchezaji huyo alishiriki kikamilifu kwenye mazoezi ya timu hiyo kwa mara ya kwanza tangu ajikute katika tuhuma za udhalilishaji.
“Ametoa ushirikiano kikamilifu, Antony anaweza akacheza lakini Jumapili ilikuwa siku yake ya kwanza kwenye mazoezi ya timu, kuna mazoezi ya mwisho Jumatatu na baada ya hapo tutaamua, yupo katika hesabu zetu,” alisema Ten Hag.
Wasichana wanaodai kudhalilishwa na Antony mbali na Gabriela wengine ni Rayssa de Freitas na Lana ambao wote waliwasilisha tuhuma hizo kwenye chombo kimoja cha habari nchini Brazil ingawa mchezaji huyo amekana tuhuma zote hizo.
Antony anasubiriwa kwa hamu na mashabiki wa Man United leo Jumanne ili acheze mechi yake ya kwanza tangu kuibuka kwa tuhuma hizo.
Mechi za leo Jumanne Ligi ya Mabingwa Ulaya
Kundi A
FC Copenhagen v Bayern Munich
Man United v Galatasaray
Kundi B
Lens v Arsenal
PSV Eindhoven v Sevilla
Kundi C
Union Berlin v Sporting Braga
Napoli v Real Madrid
Kundi D
FC Red Bull v Real Sociedad
Inter Milan v Benfica
Mechi za kesho Jumatano Ligi ya Mabingwa Ulaya
Kundi E
Atlético Madrid v Feyenoord
Celtic v Lazio
Kundi F
Borussia Dortmund v AC Milan
Newcastle v PSG
Kundi G
Red Star Belgrade v Young Boys
RB Leipzig v Man City
Kundi H
Royal Antwerp v Shakhtar Donetsk
FC Porto v Barcelona
