
Na mwandishi wetu
Aliyewahi kuwa mfadhili wa Simba SC, Azim Dewji ameiomba klabu hiyo kuhakikisha msimu huu wanafika hatua ya nusu fainali au fainali katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Jumapili iliyopita, Simba ilitinga hatua ya makundi ya michuano hiyo ikiwa ni mara ya tano katika miaka ya karibuni, kitu ambacho Dewji ameeleza kuwa ni cha kawaida kwao kwa sasa na hakuna kipya cha zaidi.
“Niupongeze uongozi wa Simba kwa jitihada za kujenga timu imara na mazoea ya kufika robo fainali kwa misimu mitano iliyopita kwenye mashindano ya Caf (Shirikisho la Soka Afrika), lakini kwa uzoefu waliokuwa nao nadhani msimu huu wanapaswa kufika mbali zaidi na ninaamini uwezo huo wanao,” alisema Dewji.
Alisema ingawa anatambua ugumu uliopo kwenye michuano hiyo lakini kwa uzoefu walionao anaamini hakuna kinachoshindikana, kikubwa ni kuwepo kwa mikakati mizuri ya uongozi na benchi la ufundi na wachezaji kutimiza majukumu yao ipasavyo.
Wekundu hao walifanikiwa kutinga makundi baada ya sare ya bao 1-1 dhidi ya Power Dynamos ya Zambia kwa faida ya mabao ya ugenini baada ya mchezo wa awali wa ugenini kuisha kwa sare ya mabao 2-2.
