Madrid, Hispania
Aliyekuwa kocha wa timu ya wanawake ya Hispania, Jorge Vilda anachunguzwa na polisi akihusishwa katika kashfa ya udhalilishaji inayomkabili aliyekuwa rais wa Shirikisho la Soka Hispania (RFEF), Luis Rubiales.
Vilda aliyeiwezesha timu hiyo kubeba Kombe la Dunia la Wanawake (WWC) Agosti mwaka huu, alifutwa kazi hivi karibuni ikiwa ni mwendelezo wa kukabiliana na sakata linalomkabili Rubiales ambaye naye alilazimika kuachia ngazi.
Rubiales alizua taharuki na kujikuta akijadiliwa duniani kote baada ya kumbusu mdomoni mshambuliaji wa timu ya Hispania, Jenni Hermoso ambaye baadaye alisema hakuwa na makubaliano ya kupigwa busu hilo.
Hata hivyo Rubiales ambaye ametakiwa kutomsogelea Jenni kwa umbali wa mita 200, alikana kufanya kosa lolote la udhalilishaji badala yake alisema alichokifanya kilitokana na furaha iliyopitiliza na kulikuwa na makubaliano.
Baada ya kukamatwa na kuhojiwa, Vilda sasa atatakiwa kuripoti mahakamani Oktoba 10 ili kujibu tuhuma zinazohusu uhusika wake katika sakata la Rubiales ambaye pia anadaiwa kuwa ni mshirika wake wa karibu.
Wengine ambao vyombo vya usalama nchini Hispania vinawachunguza ni pamoja na Albert Luque ambaye ni mkurugenzi wa timu ya soka ya wanaume ya Hispania pamoja na mkurugenzi wa masoko wa RFEF, Ruben Rivera.
Timu ya wanawake ya Hispania iliyokuwa katika mgomo wa kumpinga Rubiales hatimaye imefuta mgomo huo na juzi Jumanne ilipata ushindi wa mabao 5-0 mbele ya Switzerland
Kimataifa Kocha wa wanawake Hispania matatani
Kocha wa wanawake Hispania matatani
Read also
