Na mwandishi wetu
Meneja wa Habari na Mawasiliano Simba SC, Ahmed Ally ameeleza kuwa beki wao wa kati, Henock Inonga ataukosa mchezo wa marudiano dhidi ya Power Dynamos ya Zambia utakaopigwa kwenye uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, Oktoba Mosi, mwaka huu.
Ameeleza kuwa Inonga ataendelea kusalia nje ya uwanja kwa takriban siku 10 zaidi akiuguza jeraha lake la mguu wa kulia alilolipata kwenye mchezo wao dhidi ya Coastal Union uliopigwa wiki iliyopita.
Wengine wataokosa mechi hiyo ya marudiano ya raundi ya kwanza ya kuwania kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ni kipa Aishi Manula anayetarajia kurejea dimbani Oktoba, mwaka huu na Aubin Kramo anayeendelea kupatiwa matibabu.
“Tunafahamu mchezo ni mgumu dhidi ya Power Dynamos, wote mliona namna walivyotusumbua lakini wanakuja nyumbani Tanzania, sehemu ambayo hakuna aliyetoka salama na hicho ndicho watakutana nacho,” alisema Ally.
Alisema anaamini wataingia hatua ya makundi na hilo ni jambo la kawaida kwao, kwani wameshaingia zaidi ya mara tatu na kuishia hatua ya robo fainali kwenye miaka mitano iliyopita.
Kwa mujibu wa ofisa huyo, Dynamos inatarajiwa kuwasili nchini kesho Alhamisi majira ya saa 12 jioni huku waamuzi wa mtanange huo wakitarajiwa kutua nchini Septemba 30, mwaka huu.
Katika mechi ya kwanza iliyopigwa kwenye Uwanja wa Levy Mwanawasa, Ndola, timu hizo zilitoshana nguvu kwa sare ya mabao 2-2.
