Na mwandishi wetu
Kiungo wa timu ya taifa, Taifa Stars, Baraka Majogoro (pichani) anayechezea Chippa United ya Afrika Kusini amepewa tuzo ya mchezaji bora wa mechi yao na Super Sport United katika Ligi Kuu ya Afrika Kusini.
Katika mchezo huo wa juzi Chippa United ilishinda kwa bao 1-0 na kukwea hadi nafasi ya nne ikifikisha pointi 12 katika msimamo wa ligi hiyo wakiongozwa na Mamelodi Sundown, Golden Arrow FC na Super Sport ipo nafasi ya tatu.
Akihojiwa baada ya mchezo huo Majogoro alisema mechi ilikuwa ngumu na yenye ushindani lakini wanashukuru kwa kupata matokeo mazuri.
“Nashukuru kwa tuzo niliyopata pia, mchezo haukuwa rahisi lakini tumepambana na kupata ushindi, halikuwa jambo jepesi kulingana na ushindi uliokuwepo muda wote uwanjani,” alisema.
Majogoro anayejumuishwa mara kwa mara kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania au Taifa Stars amekuwa na kiwango bora tangu kujiunga na timu hiyo akitokea KMC aliyokuwa akiitumikia msimu uliopita.
