Na mwandishi wetu
Mchezaji nyota wa mpira wa kikapu, Hasheem Thabit amerejea nchini Tanzania na kujiunga na timu ya Pazi kwa ajili ya michezo ya hatua za awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika (BAL) inayotarajiwa kuchezwa Dar es Salaam kuanzia Oktoba 10 hadi 15, mwaka huu.
Tanzania itakuwa mwenyeji wa michuano hiyo kwa mara ya pili, hatua ya makundi ikiwakilishwa na bingwa wa taifa, Pazi watakaoungana na mabingwa wengine kuwania kucheza hatua ya mtoano katika Kundi D pamoja na Dynamo BC ya Burundi, K.P.A ya Kenya na Sebeta City ya Ethiopia.
Akizungumzia ujio wake Thabiti alisema: “Si mimi pekee, na timu ya Pazi kwa ujumla, lengo langu kubwa kurudi nyumbani ni kuja kufanya kikapu katika kiwango ambacho Tanzania inatakiwa icheze.”
Alisema mashabiki wategemee mabadiliko katika mchezo wa kikapu kwani kwa miaka mingi wanashiriki ila hawafiki mbali na sasa muda umewadia kuonesha kikapu katika kiwango kingine.
Thabit (pichani juu) kabla ya kuanza kucheza kikapu kimataifa na kuwa mchezaji wa kulipwa aliwahi kuzichezea timu za Outsiders na Makongo Sekondari na mwaka 2009 aliingia kwenye Ligi ya Kikapu ya Marekani (NBA) akichezea Memphis Grizzlies.
Thabit alidumu NBA hadi mwaka 2015 akicheza klabu tofauti na mwaka 2017 akajiunga na Yokohama B-Corsairs ya Japan kabla ya baadaye kurejea Marekani kwa mwaka mmoja na kisha akaenda China na sasa yupo The TaiwanBeer HeroBears ya Taiwan.
Wakati huo huo, timu za wanawake za Vijana Queens na JKT Stars zimefuzu kushiriki Ligi ya Wanawake Afrika inayoandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Kikapu Afrika.
Hatua ya awali ya mashindano hayo itachezwa jijini Kigali, Rwanda kuanzia Oktoba 21 mpaka 28 na fainali zitachezwa nchini Misri, Desemba, mwaka huu. Timu hizo zimefuzu moja kwa moja baada ya kufikia hatua ya fainali katika Ligi ya Taifa (NBL 2022).
Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF) linazitakia timu hizo kila la heri kwenye uwakilishi wa kupeperusha bendera ya Taifa katika mashindano hayo.
Kikapu Hasheem Thabit arejea Dar kuichezea Pazi
Hasheem Thabit arejea Dar kuichezea Pazi
Related posts
Read also
