Na mwandishi wetu
Uongozi wa Simba SC umeeleza kuridhiswa na matokeo ya timu hiyo uwanjani na kuamua kuyapa kisogo maoni mengine binafsi kuhusu kutovutia kwa soka la kikosi cha timu hiyo.
Hayo yameelezwa na Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally baada ya maoni ya baadhi ya mashabiki wa timu hiyo juu ya kutovutiwa na falsafa ya kikosi hicho chini ya kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ tangu kuanza kwa ligi msimu huu.
“Tangu tumeanza msimu tunaondoka na furaha uwanjani sababu tunapata ushindi, sasa hayo masuala ya mpira hauvutii, hauna kasi, yanabaki kuwa maoni ya watu binafsi lakini kama taasisi tunaridhishwa na kile kinachoendelea, maana tumewekeza kwa ajili ya kupata ushindi na tunaupata,” alisema Ally.
Simba pia imeshinda michezo yake mitatu ya Ligi Kuu NBC mpaka sasa ikiibabua Mtibwa Sugar mabao 4-2 kabla ya kuibonda Dodoma Jiji mabao 2-0 kisha ikaichakaza Coastal Union mabao 3-0.
Pia, Wekundu hao ambao wametwaa ndoo ya Ngao ya Jamii msimu huu, wamecheza mchezo wa mkondo wa kwanza wa raundi ya kwanza kuwania kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kupata sare ya mabao 2-2 ugenini dhidi ya Power Dynamos ya Zambia.
Akizungumzia mchezo wa marudiano, Ally alisema timu hiyo imeshaanza mazoezi tangu jana Ijumaa ikiwawinda Dynamos katika mchezo huo utakaopigwa Oktoba Mosi, mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Katika mechi hiyo, Simba inahitaji ushindi au sare isiyozidi kuanzia mabao 3-3 kwa ajili ya kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo mikubwa kwa ngazi ya klabu Afrika.
