Na mwandishi wetu
Mshambuliaji wa Coastal Union, Hija Ugando ameomba radhi kwa kitendo cha kumchezea vibaya beki wa kati wa Simba SC, Henock Inonga kwenye mechi iliyopigwa Alhamisi hii Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Katika tukio hilo lililotokea dakika ya 19 ya mchezo huo ulioisha kwa Simba kushinda mabao 3-0, Ugando alipewa kadi nyekundu na Inonga kukimbizwa hospitali kutokana na majeraha aliyoyapata.
“Natanguliza samahani sababu kila muungwana anapovuliwa nguo huchutama, binafsi sikutegemea wala sikuwahi kufanya kitendo hicho kabla. Imeniumiza na kunisikitisha sana, naomba radhi sababu mimi si muumini wa kufanya vitendo vibaya uwanjani,” alisema Ugando.
Pia imeelezwa kuwa beki huyo amesharuhusiwa kutoka hospitali kwani amepatwa na kidonda ambacho ameshonwa nyuzi 13 tofauti na ilivyodhaniwa kuwa amevunjika.
“Inonga hajavunjika, amepata kidonda pale ambapo alikanyagwa na ameshapatiwa matibabu kutoka Hospitali ya Temeke na sasa ameruhusiwa kurejea kwake, anaendelea kuuguza kidonda na tunashukuru Mungu kuona hajavunjika,” alisema Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally.
Ofisa huyo alifafanua kuwa Inonga atakaa nje kwa wiki chache kabla ya kuruhusiwa kuanza mazoezi na wenzake ikitegemeana na maendeleo ya kidonda hicho.
