Berlin, Ujerumani
Ujerumani imemteua Julian Nagelsmann mwenye umri wa miaka 36 kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa kwa mkataba utakaofikia ukomo Julai 2024 baada ya fainali za Euro 24 ambazo Ujerumani itakuwa mwenyeji.
Nagelsmann (pichani) amepewa jukumu hilo zito baada ya Flick kutimuliwa kutokana na matokeo mabaya ya Ujerumani mapema mwezi huu ikiwamo mechi ya kirafiki na Japan ambayo Ujerumani ilichapwa mabao 4-1.
Fainali za Euro 2024 zitakazofanyika kati ya Juni 14 hadi Julai 14 mwakani nchini Ujerumani, utakuwa mtihani wa kwanza kwa Nagelsmann ambaye hiyo inakuwa kazi yake ya kwanza tangu Machi mwaka huu alipotimuliwa kuinoa klabu ya Bayern Munich.
“Tuna mashindano ya Kombe la Ulaya (Euro 24) katika nchi yetu wenyewe, hilo ni jambo la kipekee, ni kitu ambacho kinatokea baada ya miaka kadhaa, nina shauku kubwa ya kuikabili hii changamoto, tutakuwa kundi imara mwakani,” alisema Nagelsmann.
Nagelsmann atakuwa na timu hiyo katika mechi yake ya kwanza dhidi ya Marekani ambayo ni ya kirafiki itakayopigwa Oktoba 14 mjini Connecticut na siku tatu baadaye timu hiyo itaumana na Mexico mjini Philadelphia.
“Julian Nagelsmann ndiye chaguo letu la kwanza wakati tunaanza kumsaka kocha wa timu ya taifa,” alisema Rudi Voller ambaye ni mkurugenzi wa michezo wa Chama cah Soka Ujerumani.
Nagelsmann, kocha mwenye umri mdogo anatajwa kuwa mmoja wa makocha wenye upeo na kipaji tangu alipoanza kuinoa Hoffenheim akiwa na miaka 28 kabla ya kujiunga RB Leipzig aliyoifikisha hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Bayern ilivutiwa na mafanikio ya kocha huyo na kuilipa Leipzig Pauni 21.7 milioni ili kuvunja mkataba wake na timu hiyo na kumsainisha mkataba wa miaka mitano akichukua nafasi ya Flick.
Akiwa Bayern, Nagelsmann amebeba taji la ligi kuu au Bundesliga katika msimu wake wa kwanza pamoja na taji la Ujerumani kabla ya kutimuliwa mwezi Machi akiwa ametoka kushinda mechi tano kati ya 10 za ligi, Chelsea na Tottenham zilihusishwa naye lakini hakuna iliyoweza kumpata.
Mara baada ya Flick kutimuliwa kuinoa Ujerumani, Voller ambaye pia ni mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo alikabidhiwa kibarua hicho kwa muda na kuiongoza timu hiyo katika mechi ya kirafiki dhidi ya Ufaransa ambayo Ujerumani ilishinda kwa mabao 2-1.
