Manchester, England
Winga wa Man United, Jadon Sancho ametakiwa kumuomba radhi kocha wake, Erik ten Hag baada ya kutofautiana naye hivi karibuni vinginevyo hatokuwa na nafasi ya kuendelea kuichezea timu hiyo.
Mchezaji huyo amepigwa marufuku kufanya mazoezi katika kikosi cha kwanza, badala yake ametakiwa kufanya mazoezi ya peke yake baada ya kudai hadharani kwamba Ten Hag aliongopa kuhusu sababu ya kumuondoa katika kikosi kilichoumana na Arsenal na kufungwa mabao 3-1.
Chanzo kimoja cha habari kiliarifu kuwa wawili hao walifanya mazungumzo mapema wiki hii lakini inadaiwa Sancho hakuwa tayari kuomba radhi hivyo huenda akaendelea na mazoezi ya peke yake.
Habari zaidi zinadai kuwa kama mchezaji huyo atashikilia msimamo wake wa kutokuwa tayari kuomba radhi mwishowe atajikuta akiuzwa katika dirisha dogo la usajili la Januari.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Ijumaa hii, Ten Hag alikataa kusema lolote kuhusu Sancho badala yake alisisitiza nia yake ya tangu mwanzo ya kuweka taratibu za kinidhamu tangu ajiunge na Man United.
“Hakukuwa na utamaduni mzuri kabla ya kuja kwangu, nilikuja hapa msimu uliopita na hivyo ilikuwa lazima kuweka taratibu za kinidhamu na hivyo ndivyo nilivyofanya na ni kazi yake kulinda taratibu hizo,” alisema Ten Hag.
Sancho aliingia katika mzozo na Ten Hag baada ya kutoa taarifa kwenye mitandao ya kijamii akipinga hoja ya kocha wake aliyesema kwamba mchezaji huyo aliondolewa katika kikosi kilichoumana na Arsenal baada ya kuzembea mazoezini.
Katika kumpinga Ten Hag, Sancho alisema kwamba kocha huyo amemtoa kafara na hakuwa mkweli kuhusu kutompa nafasi katika mechi dhidi ya Arsenal ingawa mchezaji huyo baadaye alifuta alichokiandika kwenye mitandao ya kijamii.
