Rio de Janeiro, Brazil
Mshambuliaji wa Tottenham Hotspur, Richarlison (pichani) amesema anajiandaa kutafuta msaada wa kisaikolojia atakaporudi England baada ya mapumziko ya mechi za kimataifa.
Richarlison alionekana kwenye picha mbalimbali Jumamosi iliyopita akitokwa machozi baada ya kutolewa wakati akiiwakilisha Brazil katika mechi na Bolivia ya kufuzu Kombe la Dunia 2026, mechi ambayo Brazil ilishinda kwa mabao 5-1.
Baadaye mchezaji huyo alisema kwamba hali hiyo ilimtokea kutokana na mambo ambayo yamekuwa yakijitokeza ndani na nje ya uwanja ambayo yapo nje ya taratibu zake.
Richarlison amefunga mabao manne tu katika mechi 40 alizoichezea Spurs tangu ajiunge na timu hiyo majira ya kiangazi mwaka jana akitokea Everton kwa ada ya Pauni 60 milioni.
“Nimepitia kipindi kigumu mno nje ya uwanja katika miezi hii mitano iliyopita, walau kwa sasa mambo yameanza kuwa mazuri nyumbani, watu ambao macho yao yalikuwa kwenye pesa zangu tu kwa sasa hawapo tena karibu na mimi,” alisema Richarlison.
“Mambo sasa yameanza kwenda vizuri, na naamini nitakuwa na mwendelezo mzuri Tottenham, na mambo yatawezekana kwa mara nyingine,” alisema.
“Nikirudi England naenda kutafuta msaada wa kisaikolojia kutoka kwa wataalam, ili nijiimarishe zaidi kifikra, hiyo ndiyo hali halisi, nataka kurudi katika ubora nikiwa imara,” alisema.
Richarlison alishindwa kuitumia nafasi aliyoipata katika mechi na Bolivia na baadaye kutolewa dakika ya 71 na juzi Jumanne alitolewa dakika ya 64 katika mechi dhidi ya Peru, mechi ambayo Brazil ilishinda kwa bao 1-0.
Richarlison ambaye hivi karibuni ilidaiwa ameachana na wakala wake wa siku nyingi, Renato Velasco, alisema kwamba hali ya huzuni aliyokuwa nayo haikutokana na kucheza vibaya na si kweli kwamba mechi na Bolivia ilimkataa.
“Kwa mawazo yangu sikucheza vibaya mechi na Bolivia, bali ilikuwa ni katika kuguswa na matukio ya nje ya uwanja yaliyo nje ya taratibu zangu, ambayo yamenitawala na kushindwa kujiongoza, si kwa sababu ya lolote nililofanya bali ni kwa sababu ya watu walio karibu nami,” alisema Richarlison.
Richarlison alisema kwamba anaamini atakuwa katika timu ya Brazil kwenye mechi ijayo na hilo ndilo jambo analolifanyia kazi na pia anataka kuweka mambo sawa na Spurs kwa kuzungumza na viongozi.
Brazil itacheza mechi nyingine ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Venezuela itakayopigwa Oktiba 13 na siku tano baadaye itacheza na Uruguay wakati kwenye Ligi Kuu England, Spurs ya Richarlison, Jumamosi itakuwa mwenyeji wa Sheffield United.
