Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Habibu Kondo amesema wamepanga kuchukua pointi tatu za kwanza msimu huu kwa kuwafunga Dodoma Jiji katika mchezo wa Ligi Kuu NBC utakaopigwa Ijumaa hii kwenye, Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
Mtibwa inayoshika nafasi ya 12 kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi moja haijaonja ladha ya ushindi katika mechi zake mbili za awali ilizocheza uwanja wake wa nyumbani, Manungu Complex, Morogoro.
Kocha huyo alisema mapumziko ya muda mrefu ya ligi yamemsaidia kurekebisha mapungufu ambayo aliyabaini kwenye mechi mbili walizocheza awali hivyo wanakwenda kuivaa Dodoma wakiwa imara.
“Tumezitumia vizuri wiki mbili za mapumziko, makosa yaliyosababisha tukashindwa kupata ushindi nyumbani tumeyarekebisha na tupo tayari kuanza ligi Ijumaa hii tukiwa ugenini kwa kuifunga Dodoma ingawa mchezo utakuwa mgumu,” alisema Kondo.
Kondo alisema katika mechi mbili zilizopita makosa yaliyokuwa kwenye safu ya ulinzi na ushambuliaji, wameyarekebisha na mechi za karafiki walizocheza zimewasaidia kubaini kuwa wapo tayari kwa ushindani.
Timu hiyo ilipoteza mechi yake ya kwanza ikifungwa mabao 4-2 na Simba SC kabla ya kutoa sare ya bao 1-1 dhidi ya Coastal Union ya Tanga.
