Madrid, Hispania
Beki wa timu ya Real Madrid, Dani Carvajal (pichani) amemtetea rais wa Shirikisho la Soka Hispania (REEF), Luis Rubiales aliyesimamishwa kwa kumbusu mdomoni mshambuliaji wa timu ya wanawake ya Hispania, Jenni Hermoso.
Carvajal alisema kwamba kwa sasa hawezi kusema kama Jenni alionewa au la hadi hapo taratibu za kisheria zitakapokamilika.
“Kuna vyombo husika kisheria ambavyo ndivyo vitasema kama kweli Jenni ameonewa, vyombo ambavyo kwa sasa vinaendelea na uchunguzi, vitaamua kama kuna aliyeonewa na aliyeonea,” alisema Carvajal.
Akijenga hoja yake, Carvajal ambaye pia ni beki wa timu ya taifa ya Hispania alisema kwamba kwa hali ilivyo Rubiales naye anatakiwa kuungwa mkono kama ambavyo Jenni amekuwa akiungwa mkono.
“Naweza kuelewa kwamba Jenni anapitia katika wakati mgumu, ni lazima tuoneshe mshikamano kwake lakini pia sidhani kama rais (Rubiales) anapitia wakati mzuri, siko hapa kwa ajili ya kuwa na hitimisho kwa yeyote,” alifafanua Carvajal.
Carvajal pia alisema kwamba kujenga dhana au hisia kwamba mtu fulani si mkosaji ni haki ya kikatiba na si sahihi kumkandamiza au kumshutumu mtu yeyote.
Rubiales aliingia matatani Agosti 20 mwaka huu baada ya kumbusu Jenni mdomoni kwa kile alichodai kwamba ni furaha iliyopita kifani baada ya timu ya wanawake ya Hispania kuifunga England bao 1-0 na kubeba Kombe la Dunia la Wanawake (WWC).
Tayari vyombo mbalimbali vya kisheria vimeanza uchunguzi ikiwamo ofisi ya waendesha mashitaka ya Hispania huku baadhi ya wachezaji wakigoma kuichezea timu ya taifa ya Hispania kama kiongozi huyo ataendelea kuwa madarakani.
Fifa imemsimamisha Rubiales kwa siku 90 wakati uchunguzi ukiendelea ingawa mwenyewe amekataa kujiuzulu akidai hajafanya kosa lolote na kulikuwa na makubaliano kwa alichokifanya ingawa Jenni amepinga hoja hiyo.
