Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Singida Fountain Gate, Ernst Middendorp (pichani) ameanza kujiwinda na mchezo ujao wa Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuimarisha zaidi safu ya kiungo baada kuuona ubora wa wapinzani wake, Future FC ya Misri.
Singida ipo jijini Dar es Salaam ikiendelea na kambi ya maandalizi ya mchezo huo wa raundi ya kwanza ya michuano hiyo unaotarajiwa kuchezwa Septemba 17, mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Middendorp aliyetua hivi karibuni kuchukua mikoba ya Hans Pluijm, ameanza kuyafanyia kazi mapungufu ya kikosi chake huku akiwafuatilia kwa ukaribu nyota hatari wa Future akiwemo Ahmed Refaat mwenye uwezo wa kucheza winga zote mbili na kiungo mshambuliaji.
“Nimefanikiwa kuwafuatilia Future kwa kuona ubora wao, wapinzani wetu wako imara kwenye safu ya kiungo na wana vijana ambao wamekuwa akisumbua sana kwenye mechi zilizopita.
“Tunaendelea kufanyia kazi mapungufu ya timu yaliyojitokeza katika mechi zilizopita ili kufanya vizuri kwenye mechi dhidi ya Future na kusonga mbele. Wapinzani ni wazuri kwa hiyo tunajiandaa vizuri na tutaingia uwanjani kwa kuwaheshimu kulingana na ubora walionao,” alisema Middendorp.
Singida imetinga hatua hiyo baada ya kuisukuma nje JKU ya Zanzibar kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-3. Mechi ya kwanza Singida ilishinda mabao 4-1, mechi ya pili iliruhusu kufungwa mabao 2-0.
Soka Middendorp aimarisha kiungo Singida FG
Middendorp aimarisha kiungo Singida FG
Read also
