Paris, Ufaransa
Oktoba 30 mwaka huu mshindi wa tuzo ya Ballon d’Or atatangazwa huku majina ya washambuliaji Lionel Messi na Erling Haaland, mmoja wao akipewa nafasi kubwa ya kubeba tuzo hiyo.
Messi ambaye kwa sasa anaichezea Inter Miami ya Marekani na Haaland wa Man City wamo katika orodha ya wachezaji 30 ambao mmoja wao anaweza kubeba tuzo hiyo ingawa mafanikio ya wawili hao yanasimama juu ya wachezaji wengine 28 wanaokamilisha orodha hiyo.
Kwa Messi iwapo atabeba tuzo hiyo safari hii atakuwa amefanya hivyo kwa mara ya nane na kuwa juu ya Cristiano Ronaldo anayeshika nafasi ya pili akiwa amebeba tuzo hiyo mara tano.
Jina la Messi lilikosekana katika orodha ya wanaowania tuzo hiyo mwaka jana, safari hii ameingia akibebwa na mafanikio ya timu yake ya taifa ya Argentina ambayo mwishoni mwa mwaka jana ilibeba Kombe la Dunia katika fainali zilizofanyika Qatar.
Katika klabu mambo hayakuwa mazuri kwa Messi msimu uliopita, klabu yake ya PSG kitu pekee inachojivunia ni taji la Ligi 1 Ufaransa, ilikwama katika Ligi ya Mabingwa Ulaya ikitolewa katika hatua ya 16 bora.
Katika msimu huo, Messi baada ya kuiwakilisha Argentina kwenye fainali za Kombe la Dunia na kubeba taji alimalizia msimu wa Ulaya kabla ya kutimkia nchini Marekani kujiunga na Inter Miami akiwa mchezaji huru na tayari ameiwezesha timu hiyo Kombe la Ligi na kufuzu fainali za US Open.

Haaland anayetajwa kuwa mpinzani mkuu wa Messi katika kuwania tuzo hiyo, msimu uliopita aliifungia Man City mabao 52 katika mechi 53 za mashindano mbalimbali, mabao ambayo yalikuwa na mchango mkubwa kwa timu hiyo kubeba mataji matatu (treble) makubwa ya Ligi Kuu England (EPL), FA na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Haaland, 23, pia ametwaa tuzo kadhaa England huku akiweka rekodi ya kipekee ya kufunga mabao 36 katika msimu wake wa kwanza wa Ligi Kuu England.
Orodha kamili ya wanaowania Ballon d’Or ni kama ifuatavyo…
Andre Onana – Man United
Josko Gvardiol – Man City
Karim Benzema – Al Ittihad
Jamal Musiala – Bayern Munich
Mohamed Salah – Liverpool
Jude Bellingham – Real Madrid
Bukayo Saka – Arsenal
Randal Kolo Muani – PSG
Kevin De Bruyne – Man City
Bernardo Silva – Man City
Emiliano Martínez – Aston Villa
Khvicha Kvaratskhelia – Napoli
Rúben Dias – Man City
Nicolo Barella – Inter Milan
Erling Haaland – Man City
Yassine Bounou – Al Hilal
Martin Ødegaard – Arsenal
Julian Álvarez – Man City
Ilkay Gundogan – Barcelona
Vinícius Junior – Real Madrid
Lionel Messi – Inter Miami
Rodri – Man City
Lautaro Martínez – Inter Milan
Antoine Griezmann – Atletico Madrid
Robert Lewandowski – Barcelona
Kylian Mbappé – PSG
Kim Min-jae – Napoli
Victor Osimhen – Napoli
Luka Modric – Real Madrid
Harry Kane – Bayern Munich
