Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’, amempongeza kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Luis Miquissone kwa kupungua uzito akisema hilo ni jambo zuri kuelekea mchezo wa raundi ya kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Power Dynamos.
Miquissone aliyetua Simba kwa mara ya pili mwanzoni mwa msimu huu akitokea Al Ahly ya Misri, ameonekana kutokuwa kwenye kiwango chake kilichozoeleka kutokana na uzito alionao sasa tofauti na awali.
“Miquissone alikuja akiwa na uzito wa kilo 77, lakini kumpa program maalumu ya kupunguza uzito na mwili kwa sasa amepungua mapaka kilo 73, amekuwa mwepesi kuliko kawaida na amerudi kwenye kiwango chake kile cha zamani, naamini atakuwa msaada mkubwa kwenye mechi za kimataifa zinazotukabili,” alisema Robertinho.
Mbali na Miquissone, kocha huyo pia alifurahishwa kupona majeraha kwa Aubin Kramo, sanjari na kipa namba moja wa timu hiyo, Aishi Manula ambaye naye ameanza mazoezi mepesi wiki iliyopita akitarajiwa kujiunga na mazoezi ya kikosi siku chache za usoni.
