Na mwandishi wetu
Hatimaye kipa namba moja wa Simba, Aishi Manula amepiga hatua muhimu kwa kuanza rasmi mazoezi ya uwanjani baada ya kuuguza jeraha la nyama za paja alilofanyiwa upasuaji takriban miezi mitatu iliyopita.
Manula ameanza mazoezi hayo kwenye Uwanja wa Mo Simba Arena, Dar es Salaam chini ya usimamizi wa timu ya wataalamu wa viungo na tiba ya timu hiyo, ikielezwa kuwa kipa huyo amefikisha zaidi ya asilimia 80 ya kuwa fiti kama awali.
Daktari wa Simba, Edwin Kagabo alitoa ufafanuzi kuwa baada ya Manula kumaliza awamu ya kwanza ya upasuaji, ya pili ya mazoezi tiba, sasa wako hatua ya tatu ya kumpa mazoezi ya sehemu ya nyama aliyoumia ili akae sawa kabisa na maendeleo yamekuwa mazuri.
“Maendeleo ni mazuri na yanaridhisha kwa kiwango kikubwa, anaridhisha sasa kurudi uwanjani, lengo kubwa la awamu ya tatu ni kufanya mazoezi katika ile nyama iliyopata jeraha na kwa maendeleo tuko asilimia 80 kuelekea 90 ya kupona kabisa,” alisema Kagabo.
Manula alipata majeraha hayo Aprili 7 kwenye mechi ya robo fainali ya Kombe la FA (ASFC) dhidi ya Ihefu na kufanyiwa upasuaji Juni 2, mwaka huu.
Kurejea kwa Manula kutaifanya Simba iwe na makipa watano baada ya Ally Salim, Ayoub Lakred aliyesajiliwa kutoka FAR Rabat ya Morocco, Ahmed Feruz aliyepandishwa kutoka kikosi cha vijana na Hussein Abel aliyetua kutoka KMC.
