Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Mbeya City inayoshiriki Ligi ya Championship, Salum Mayanga amesema licha ya kuwa na kazi ngumu mbele yao lakini wamepania kuhakikisha wanairejesha timu hiyo Ligi Kuu NBC msimu ujao.
Mayanga ameyasema hayo wakati kikosi chake kikiendelea na maandalizi ya kuivaa Green Warriors katika mchezo wa kwanza wa ligi hiyo itakayoanza Septemba 9, mwaka huu.
“Tuko kwenye maandalizi mazuri, tumefanya usajili wa wachezaji vijana na wazoefu ukiwa ni mchanganyiko ambao tumekuwa nao mazoezini kwa takriban wiki mbili na umetupa picha nzuri kuelekea mechi ya kwanza na Green Warriors.
“Niseme kuna kazi ngumu ya kufanya mbele ya safari lakini ni lazima tuifanye na tuwe kwenye hali ya kupambana kuirejesha timu ligi kuu msimu ujao, hiyo ndio nia ya uongozi, mimi na wenzangu wa benchi la ufundi,” alisema Mayanga kocha wa zamani wa Mtibwa Sugar.
Kocha huyo pia alisema anaamini cha muhimu ni ushirikiano baina ya benchi la ufundi, mashabiki na wakazi wa Mbeya kwa ujumla kuhakikisha timu hiyo iliyodumu kwenye ligi kuu kwa misimu 10 mfululizo kabla ya kushuka mwishoni mwa msimu uliopita, inarejea kwa kishindo msimu ujao.
