Na mwandishi wetu
Beki wa Yanga, Nickson Kibabage ameongezwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa, Taifa Stars kinachojiandaa kuivaa Algeria Septemba 7, mwaka huu.
Kibabage, beki wa kushoto mwenye jicho la kushambulia ameongezwa ikiwa siku mbili zimepita tangu kutangazwa kwa kikosi hicho kilicho chini ya Kocha Adel Amrouche.
Leo Ijumaa Yanga ilieleza juu ya beki huyo kuitwa katika kikosi hicho na kufafanua kuwa tayari mchezaji huyo alishaanza safari hiyo akielekea Tunisia kujiunga na Stars iliyoweka kambi nchini humo.
“Beki wetu wa kushoto ameongezwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania na tayari ameanza safari ya kuelekea Tunisia kujiunga na kambi ya timu hiyo. Kila la heri Kibabage,” ilieleza taarifa ya Yanga iliyowekwa kwenye kurasa zao mitandaoni.
Kuongezeka kwa Kibabage kunatoa wigo mpana kwa Amrouche kufanya uchaguzi kutokana na uwepo wa wachezaji wengine wanaomudu majukumu ya beki wa kushoto kwa ufasaha kama Novatus Dismas na Abdi Banda.
Kiwango cha Kibabage alichoonesha kwenye mechi mbili zilizopita dhidi ya Asas Djibout waliyoshinda 5-1 na ya JKT Tanzania waliyoshinda 5-0 kimetosha kumpa nafasi katika kikosi cha Stars.
Katika mechi hizo beki huyo alitoa pasi moja ya bao kwa kila mechi huku akicheza kwa kiwango kilichovutia wengi.
Soka Kibabage aitwa Stars
Kibabage aitwa Stars
Read also
