London, England
Rais wa Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa) Aleksander Ceferin (pichani) amepuuza kinachoitwa ushindani na tishio kutoka ligi ya soka Saudi Arabia ‘Saudi Pro Ligi’ akiifananisha ligi hiyo na ile ya China iliyokuja juu mwishowe ikakwama.
Katika siku za karibuni, wachezaji mastaa wa Ulaya wamekuwa wakikimbilia Saudi Arabia baada ya kutangaziwa mikataba minono yenye fedha nyingi.
Ceferin hata hivyo amesema kwamba makosa yaliyofanywa katika Ligi ya China ni hayo hayo ambayo sasa yanafanywa na Saudi Arabia na kwamba hiyo si namna nzuri.
“Walinunua wachezaji wanaoelekea mwisho kwenye soka kwa kuwatangazia pesa nyingi, soka la China halikuendelea na mwisho wa yote China hawakufuzu Kombe la Dunia,” alisema Ceferin.
Hii ni mara ya pili kwa Ceferin kutoa kauli hiyo akionekana kutoihofia Saudi Arabia ingawa watu wengine wamekuwa na hisia tofauti kuhusu nchi hiyo hasa inapolinganishwa na China.
China iliutikisa ulimwengu wa soka kwa fujo kwa kusajili wachezaji mastaa wa Ulaya kabla ya kuanza kukwama mwaka 2017 na hadi sasa jambo hilo halipo tena.
Saudi Arabia nayo inahofiwa kuangukia katika mtego wa China licha ya kuelezwa kuwa mbali na kutoa fedha nyingi za usajili, nchi hiyo pia ina mipango ya muda mrefu ya uwekezaji katika soka la vijana na imemteua Michael Emenalo kuwa mkurugenzi wa soka anayesimamia mipango ya maendeleo ya vijana.
Kocha wa Man City, Pep Guardiola ambaye wachezaji wake wawili nyota Riyad Mahrez na Aymeric Laporte wametimkia Saudi Arabia amesema nguvu ya fedha ya nchi hiyo imebadili soko la uhamisho wa wachezaji na kuzitaka klabu kubwa Ulaya kuwa makini na kinachoendelea.
Kwa upande wake, mkurugenzi mkuu wa Ligi Kuu England (EPL), Richard Masters amesema kwamba umaarufu unaojitokeza katika soka la Saudi Arabia hauwezi kumfanya awe na hofu kwa sana.
Kimataifa Rais Uefa apuuza kinachoendelea Saudi Arabia
Rais Uefa apuuza kinachoendelea Saudi Arabia
Read also
