Na mwandishi wetu
Azam FC imeeleza kuumizwa mno baada ya kutolewa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, ikikiri kuwa imewaumiza pia Watanzania wengi lakini imeahidi kujipanga zaidi kwa msimu ujao.
Hayo yameelezwa leo Jumamosi na Ofisa Habari wa Azam, Thabiti Zakaria (pichani) akifafanua kuwa kilichotokea ni funzo kwao na kimeshatokea kwa timu nyingi miaka ya nyuma hivyo sasa ni zamu yao.
Katika mechi hiyo ya hatua ya awali, Azam ilifungwa na Bahil Dar Kenema ya Ethiopia kwa penalti 4-3 kwenye Uwanja wa Azam, Complex, Dar es Salaam jana baada ya sare ya jumla ya mabao 3-3 kutokana na kila timu kushinda nyumbani mabao 2-1.
“Tunawapongeza wapinzani wamecheza vizuri, timu yao ni nzuri sana sio kwamba ukifika tu unaifunga, hapana. Inauma sana kupoteza nyumbani lakini ndio mpira uko hivyo maana hakuna timu isiyowahi kufungwa nyumbani.
“Hizi nyakati za maumivu kila timu imepitia, watu wasicheke leo tu lakini wamepitia hizi nyakati miaka tofauti tofauti kwa hiyo leo imekuwa kwetu na tunapokea hizo changamoto, najua watatulaumu wengi, wengine tumewaumiza moyo, tumeumia pamoja,” alisema Zakazi.
Alisema kuwa kama uongozi hawawezi kurudi nyuma isipokuwa sasa wanaangalia wanafanyaje baada ya hapo ili kufanya vizuri wakati ujao akieleza kuanguka sio tatizo kwao, tatizo ni kushindwa kuinuka tena.
Hata hivyo, timu hiyo imerejea mazoezini kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wake unaofuata wa Ligi Kuu NBC utakaochezwa Jumatatu hii dhidi ya Tanzania Prisons kwenye dimba la Azam Complex, Chamazi, jijini Dar es Salaam.
Soka Azam FC yaumia, yajipanga msimu ujao
Azam FC yaumia, yajipanga msimu ujao
Read also
