Manchester, England
Beki wa zamani wa Man United, Gary Neville amekerwa kwa jinsi klabu hiyo inavyochunguza sakata la mshambuliaji Mason Greenwood ambaye Februari mwaka huu alifutiwa mashtaka ya udhalilishaji kijinsia na jaribio la kubaka.
Neville (pichani juu), beki wa zamani wa kulia na ambaye kwa sasa ni mchambuzi wa soka amesema klabu hiyo imeliendesha suala hilo katika namna ya hovyo na kumekosekana uongozi imara katika kulisimamia jambo hilo.
Greenwood, 21, anatarajia kuondoka Man United kwa makubaliano ya pande mbili baada ya uchunguzi wa takriban miezi sita unaofanywa na klabu hiyo kukamilika.
“Ilikuwa wazi tangu siku ya kwanza kwamba asingeweza kuichezea tena Manchester United,” alisema Neville ambaye mbali na Man United pia alikuwa beki wa timu ya Taifa ya England.
“Tukio zima limeendeshwa hovyo, unapokuwa na mazingira kama haya kunahitajika uongozi imara na wenye maamuzi, na huo unatoka kwa viongozi wa juu, Manchester United hawana watu hao,” alisema Neville.
Greenwood (pichani chini) ambaye pia ni mshambuliaji wa timu ya Taifa ya England, alikamatwa Januari 2022 baada ya kuwapo tuhuma za udhalilishaji kijinsia ambazo pia zilichapishwa kwenye mitandao ya kijamii.
Katika taarifa yake, Greenwood alikubali kuwa alifanya makosa na anastahili kubeba lawama lakini hapo hapo alisema kwamba hakufanya makosa ambayo anatuhumiwa kuyafanya.
Man United katika taarifa yao walidai kuwa kwa kuzingatia ushahidi walio nao wamefikia hitimisho kwamba yaliyochapishwa kwenye mitandao hayatoi picha ya Greenwood kutohusika na makosa ambayo awali alishitakiwa akidaiwa kuyafanya.

Taarifa hiyo pia iliongeza kuwa watu wote waliohusishwa katika kuutafuta ukweli akiwamo Mason mwenyewe wamebaini ugumu wa mchezaji huyo kuendelea na maisha yake ya soka katika klabu ya Manchester United.
Awali ilielezwa kwamba hatma ya mchezaji huyo ingejulikana kabla ya Agosti 14 siku ambayo Man United ilicheza mechi yake ya kwanza ya msimu mpya wa Ligi Kuu England dhidi ya Wolves lakini haikuwa hivyo kwa kinachodhaniwa kuwa ni mjadala mkali baina ya vigogo wa klabu hiyo kuhusu uwezekano wa kumrudisha Greenwood Man United.
Makundi ya wanawake wa klabu ya Man United wanaongoza kampeni ya kupinga uwezekano wa mchezaji huyo kurudishwa na kuendelea na maisha ya soka katika klabu hiyo.
