Na mwandishi wetu
Baada ya kubeba Ngao ya Jamiii, Simba imeanza na ushindi katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu NBC ikiichapa Mtibwa Sugar mabao 4-3, mechi iliyopigwa Alhamisi hii jioni kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro.
Simba licha ya kupata ushindi na kuondoka na pointi tatu muhimu, mechi ilikuwa ngumu kwao na ilikuwa bado kidogo wapoteze pointi hizo kwa kile kilichoonekana kuwa ni kuyumba kwa safu ya ulinzi ya timu hiyo.
Simba ndio waliokuwa wa kwanza kupata mabao yaliyofungwa na Jean Baleke akimalizia kazi nzuri ya Kibu Dennis akiinasa pasi ambayo ilionekana kumilikiwa na Clatous Chama lakini kiungo huyo fundi akaachana na mpira huo kwa makusudi.
Kasi ya Simba ilizaa tena matunda katika dakika ya tisa kwa bao la pili lililofungwa na Willy Onana ambaye alifumua shuti akiwa kwenye lango la Mtibwa baada ya kutokea piga nikupige ambayo hatimaye ikawa na manufaa kwa Simba.
Mabao hayo yaliibua matumaini ya Simba kutoka na ushindi huo au zaidi lakini mambo yakaanza kubadilika hadi kuacha maswali kuhusu uimara wa safu ya ulinzi ya Simba hasa kwa namna ambavyo Mtibwa ilisawazisha mabao hayo kwa haraka haraka.
Mtibwa iliandika bao la kwanza katika dakika ya 20 ikineemeka na makosa ya beki mpya wa Simba, Che Malone ambaye alitaka kumpiga chenga mchezaji wa Mtibwa katika eneo la hatari lakini alinyang’anywa mpira na baadaye kuwa rahisi kwa Matheo kuujaza wavuni.
Matheo hakuwachelewesha Simba kwani dakika mbili baadaye aliipatia Mtibwa bao la pili baada ya kumzidi ujanja beki na nahodha wa Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ aliyeshindwa kuizuia pasi ndefu ya Nickson Mushi.
Timu hizo ziliendelea kushambuliana na kuufanya mchezo uwe mgumu kutabiri kabla ya Simba kuandika bao la tatu lililofungwa na Fabrice Ngoma akiujaza wavuni mpira kwa kichwa baada ya kuitumia vizuri pasi ya Baleke.
Dakika sita kabla ya mpira kumalizika, Simba waliandika bao la nne lililofungwa na Chama ambaye aliujaza mpira wavuni akiitumia pasi ya Tshabalala.
Ushindi huo umeifanya Simba kushika nafasi ya pili katika Ligi Kuu NBC ikitanguliwa na Azam ingawa zote zina pointi tatu lakini Azam ina faida ya mabao manne iliyoyapata katika mechi yake na Kitayosce.
Kwa Matheo mabao yake mawili yanamfanya kushika nafasi ya pili kwa wafungaji katika ligi hiyo akiwa ametanguliwa na Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam mwenye mabao matatu.
Soka Simba yaanza vizuri Ligi Kuu NBC
Simba yaanza vizuri Ligi Kuu NBC
Read also
