London, England
Liverpool imeibwaga Chelsea na kubeba Kombe la FA katika mechi ngumu iliyopigwa kwenye dimba la Wembley usiku huu huku timu hizo zikimaliza dakika 90 bila kufungana.
Baada ya dakika 90 kumalizika bila bao, timu ziliingia uwanjani tena kwa dakika nyingine 30 ambazo pia zilimalizika bila kufungana na ndipo sheria ya mikwaju ya penalti ilipotumika na Liverpool kuibuka na ushindi wa mabao 6-5.
Kwa ushindi huo, Liverpool sasa inakuwa imebeba taji la pili msimu huu baada ya Kombe la Ligi ililolibeba kwa kuitoa Chelsea kwa penalti 11-10 baada ya mechi kumalizika kwa timu hizo kutofungana na sasa inasubiri taji la Ligi Kuu England na lile la Ligi ya Mabingwa Ulaya ili kuweka rekodi ya kipekee ya kubeba mataji manne kwa msimu mmoja.
Kwenye Ligi Kuu England, timu hiyo inapambana na Man City katika mbio za taji la ligi hiyo huku zikiwa zimebakia mechi mbili lakini pia ina kibarua kigumu mbele ya Real Madrid katika mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya itakayopigwa Mei 28 mwaka huu. Liverpool hata hivyo pamoja na ushindi huo, pia imepata pigo baada ya wachezaji wake mahiri wawili Mohamed Salah na Virgil van Dijk kuumia na haijajulikana kama watakuwa fiti kwa ajili ya kuivaa Real Madrid na kumalizia Ligi Kuu England.
Katika mikwaju ya penalti, hali nusura iwe tete kwa timu hiyo baada ya kipa, Edouard Mendy wa Chelsea kuzuia mkwaju wa penalti wa Msenegali mwenzake Sadio Mane wakati ambao bao la Mane lingekuwa na maana kubwa katika mikwaju hiyo ya penalti.
Wakati ikionekana tayari Liverpool imepeperusha ndoto yake ya mataji manne, kipa Alisson aliokoa jahazi baada ya kuokoa penalti ya Mount ambaye alijikuta katika wakati mgumu baada ya Tsimikas kuujaza mpira wavuni katika penalti ya mwisho na kuamsha shangwe kwa mashabiki wa Liverpool.
“Najivunia vijana wangu, Chelsea walikuwa vizuri lakini mwisho wa siku lazima kuwe na mshindi mmoja na safari hii ni sisi,” alisema kocha wa Liverpool Juergen Klopp baada ya ushindi wa taji hilo ambalo wanalibeba kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2006.
Wakati Liverpool wakizungumzia rekodi hiyo, Chelsea wao wana rekodi ya kuumiza ya kufikia fainali ya michuano hiyo mara ya tatu mfululizo na kupoteza, mwaka 2020 walipoteza kwa Arsenal na mwaka jana walipoteza kwa Leicester City.
Kimataifa Liverpool baba lao FA Cup
Liverpool baba lao FA Cup
Related posts
Read also
