Manchester, England
Klabu ya Manchester United itashauriana na timu yake ya wanawake kabla ya kuamua kumbakisha au kuachana na mshambuliaji wake, Mason Greenwood (pichani) aliyekuwa akikabiliwa na tuhuma za udhalilishaji kijinsia.
Awali uamuzi wa klabu hiyo kuhusu Greenwood ilitarajiwa ungetangazwa kabla ya timu hiyo kucheza mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu England (EPL) msimu wa 2023-24, Jumatatu hii dhidi ya Wolves lakini umechelewa.
Februari mwaka huu tuhuma zilizokuwa zikimkabili Greenwood za kusudio la kubaka na udhalilishaji kijinsia zilifutwa na mahakama baada ya kukosekana ushahidi wa kutosha.
Mapema Ijumaa hii kundi la mashabiki wanawake wa Man United walitangaza nia yao ya kufanya maandamano juu ya uamuzi wowote wa kumpa nafasi Greenwood, maandamano ambayo yangefanywa nje ya Uwanja wa Old Trafford kabla ya mechi ya Jumatatu.
Hoja ya mashabiki hao ni katika kuitaka klabu hiyo kutovumilia aina yoyote ya unyanyasaji dhidi ya wanawake.
Man United sasa inataka kuwashirikisha wadau muhimu wakiwamo viongozi wa timu ya wanawake ambao baadhi yao wapo nchini New Zealand na Australia zinapofanyika fainali za Kombe la Dunia za Wanawake kabla ya kuamua lolote kuhusu Greenwood.
Hata hivyo haijaweza kufahamika mara moja sakata la mchezaji huyo litafikia tamati lini ingawa zipo habari kwamba mbali na timu ya wanawake kuhusishwa kumekuwa na mazungumzo yanayoendelea ambayo pia yanaihusisha familia ya mchezaji huyo.
Greenwood alikamatwa Januari mwaka jana baada ya kutuhumiwa kwa makosa ya kutaka kubaka na udhalilishaji wa kijinsia baada ya kuwapo habari kwamba picha zake zikiwamo za video zimewekwa kwenye mitandao ya kijamii.
Badaye hata hivyo mchezaji huyo alishitakiwa kwa tuhuma za kutaka kubaka na kuwa na tabia za kibabe dhidi ya wanawake.
Kimataifa Wanawake washikilia hatma ya Greenwood Man United
Wanawake washikilia hatma ya Greenwood Man United
Read also
