Na mwandishi wetu, Tanga
Simba imefuzu fainali ya michuano ya Ngao ya Jamii kwa kuitoa Singida Fountain Gate kwa penalti 4-2 na sasa inasubiri kuumana na Yanga Jumapili hii kwenye Uwanja wa CCM Mkwakwani mjini Tanga.
Katika mechi hiyo iliyopigwa Jumatano hii usiku, timu hizo zilipambana lakini hadi filimbi ya kumaliza mchezo inapulizwa na mwamuzi Amina Kyando kuashiria kukamilika dakika 90 hakuna timu iliyoliona lango la mwenzake.
Baada ya matokeo hayo ndipo timu hizo zilipoingia katika mikwaju ya penalti na Simba kuibuka mshindi kwa penalti nne dhidi ya mbili za Singida Fountain Gate au Singida FG.
Singida FG ndio waliokuwa wa kwanza kupiga penalti ambapo mpigaji wake, Aziz Andambwile shuti lake liliokolewa na kipa Ally Salim wakati shuti la Yusuf Kagoma lilipaa. Waliofunga penalti za Singida FG ni Tchakei na Duke Abuya.
Kwa upande wa Simba penalti yao ya kwanza ilipigwa na Luis Miquissone na kujaa wavuni wakati wafungaji wengine walikuwa ni Saido Ntibazonkiza na Mzamiru Yassin.
Mosses Phiri ndiye aliyekuwa wa mwisho na bao lake lilipokewa kwa shangwe na mashabiki wa Simba ambao sasa wanasubiri kuiona timu yao ikikabiliana na hasimu wao Yanga katika mechi ambayo mshindi atabeba taji la michuano hiyo.
Awali katika dakika 90 za kawaida timu zote zilionesha ushindani mkali na kushambuliana mara kwa mara na walikuwa Singida FG walioanza mapema kuzitikisa nyavu za Simba lakini bao hilo lilikataliwa na mwamuzi.
Bao hilo lilifungwa na Maurice Chukwu akimalizia mpira uliotemwa na kipa Ally Salim kufuatia krosi ya Kelvin Kijili lakini mwamuzi alikataa bao hilo kwa madai kuwa Francis Kazadi alimchezea rafu Ally Salim kabla ya mpira kuingia wavuni.
Uamuzi wa mwamuzi huyo kutoka Morogoro uliwakera baadhi ya wachezaji wa Singida FG ambao walianza kumzonga mwamuzi huyo mara kwa mara huku baadhi ya mashabiki nao wakimsakama.
Kasi ya Singida FG kusaka bao ilionekana kwa mara nyingine katika dakika ya 33 baada ya Chukwu kuinasa pasi ya Dickson Ambundo na kufumua shuti lililopaa juu ya lango.
Dakika sita baadaye, Kibu Dennis aliuwahi mpira uliopigwa na Shomari Kapombe lakini shuti la Kibu liliokolewa vyema na kipa wa Singida FG, Beno Kakolanya.
Katika mechi hiyo timu zote zilifanya mabadiliko lakini kubwa ni hamu ya mashabiki wa Simba kutaka kumuona mshambuliaji wao Mosses Phiri akicheza ilitimia alipoingia akichukua nafasi ya Kibu ingawa mabadiliko hayo hata hivyo hayakuweza kuwapa Simba bao katika dakika 90 za kawaida.
Simba pia walimtoa Jean Baleke na kumuingiza John Bocco na Inonga ambaye aliumia alitoka na kuingia Kennedy Juma wakati Singida FG nao walimtoa Kazadi na nafasi yake kuingia Meddie Kagere.
Yanga ambao walifuzu fainali kwa kuichapa Azam mabao 2-0 wataumana na Simba wakati Azam itaumana na Singida Fountain Gate katika mechi ya kusaka mshindi wa tatu.
Kwa mara ta kwanza msimu huu, michuano ya Ngao ya Jamii imeshirikisha timu nne ambazo ni Simba, Yanga, Azam na Singida FG badala ya mbili zilizozoeleka na haijaeleweka kama utaratibu huo mpya utakuwa wa kudumu au la.
Soka Simba yaifuata Yanga fainali
Simba yaifuata Yanga fainali
Read also
