Kiungo wa kati wa Yanga, Mudathir Yahya amesema upinzani mkubwa ulioibuka kati yake na Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam FC, ulitokana na maelekezo maalumu kutoka kwa kocha mkuu wa timu hiyo, Miguel Gamondi.
Katika mchezo huo wa nusu fainali ya Ngao ya Jamii, Fei Toto, alishindwa kutamba kama yale mashuti yake aliyokuwa akiyapiga wakati akiichezea Yanga huku mara kadhaa wawili wakionekana kugongana, kukamiana na kukabana kwa nguvu.
Kiungo huyo alisema kabla ya kwenda kwenye mchezo huo walifanya kikao maalumu na kuwachambua wapinzani ikiwemo kufatilia uwezo wa mchezaji mmoja mmoja ikiwemo kubaini uwezo na madhara yao na yeye alikabidhiwa kumkaba Fei Toto.
“Kocha alinikabidhi Fei Toto akaniambia asicheze yeye wala kuichezesha timu na mimi nilitimiza jukumu alilonipa kocha wangu ndio maana Azam hawakufanya shambulizi lolote la hatari kwenye lango letu,” alisema Mudathir.
Kiungo huyo alisema anajivunia kutimiza majukumu yake vizuri kwani imemuongezea uhakika wa kupata nafasi ya kucheza chini ya kocha huyo lakini pia anaamini ameisaidia timu yake kupata ushindi katika mchezo muhimu kama huo.
Alisema mbali na yeye kufanikiwa kumdhibiti Fei lakini kilichowasaidia kushinda mchezo huo ni timu nzima kucheza kwa umakini na kufuata vyema mbinu na maelekezo waliyopewa na kocha wao.
Katika mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 na kutinga fainali ya Ngao ya Jamii itakayochezwa Jumapili hii.
